1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GHAZNI: Maafisa wa Korea waendelea na mazungumzo na viongozi wa Taliban

14 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZB

Maafisa wa Korea Kusini wanaendelea kuzungumza na viongozi wa Taliban kwa njia simu kujaribu kuwaokoa mateka 19 ambao bado wanazuiliwa na wanamgambo wa kundi hilo nchini Afghanistan.

Baada ya siku nne za mazungumzo ya ana kwa ana, kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu imesema hakuna mazungumzo mengine yaliyopangwa kufanyika kati ya maafisa wa Korea Kusini na viongozi wa Taliban.

Mateka wawili wanawake wanajiandaa kuondoka Afghanistan kurejea nyumbani baada ya kuachiliwa huru.

Msemaji wa kundi la Taliban amesema wanawake hao wameachiwa kama ishara ya ukarimu, baada ya kuwazuilia kwa zaidi ya wiki tatu.

Tayari kundi hilo limewaua mateka wawili likitaka wafungwa wa Taliban waachiwe huru kutoka gerezani.

Wakati huo huo, mwanamume aliyejitambulisha kuwa mjerumani anayeshikiliwa na Taliban nchini Afghanistan amesema kwa njia ya simu kwamba watekaji nyara wametishia kumuua.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani imesema maafisa wake wanaendelea na juhudi za kumuokoa raia wake anayezuiliwa nchini Afghanistan.