1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gates ziarani China

Admin.WagnerD10 Januari 2011

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates, yuko China kuimarisha mahusiano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili. Yeye na mwenzake wa China, Jenerali Liang Guanglie, wamepuuzia uvumi wa kuwepo hali ya uadui baina yao.

https://p.dw.com/p/zvup
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates (kushoto) akipeana mikono na mwenzake wa China, Jenerali Liang Guanglie, baada ya kumalizika kwa mkutano wao na waandishi wa habari, Jumatatu 10 Januari 2011.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates (kushoto) akipeana mikono na mwenzake wa China, Jenerali Liang Guanglie, baada ya kumalizika kwa mkutano wao na waandishi wa habari, Jumatatu 10 Januari 2011.Picha: AP

Waziri Robert Gates yuko China, taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi Kusini ya Bara la Asia, na ambalo sasa linainukia kuyapiku mataifa ya Magharibi.

Ziara hii ya sasa, inakuja huku uvumi ukienea kuwa ushirikiano wa kijeshi baina ya mataifa haya, unadhoofika. Miongoni mwa mambo yanayozitafautisha nchi hizi, ni lile la Marekani kuizuia silaha za kijeshi Taiwan, nchi ambayo China inatambua kuwa ni jimbo lake.

Katika mkutano wa leo baina yao na waandishi wa habari, Waziri wa Ulinzi wa China, Jenerali Liang Guanglie, amesema kwamba jambo hili haliwezi kuwa na muafaka baina yao.

"Msimamo wa China uko wazi na haujabadilika. Tunalipinga moja kwa moja jambo hili." Amesema Liang.

Lakini Waziri Gates, akasema, hakuna tafauti isiyoweza kuzungumzika, na kwamba Marekani imejitolea kuimarisha mahusiano haya, katika ngazi ya kijeshi.

"Tunakubaliana sana kwamba ili kupunguza uwezekano wa kutokuwepo maelewano, mawasiliano au mashirikiano kati yetu, ni muhimu kwa mafungamano yetu ya kijeshi yawe ya kudumu na yasiathiriwe na mambo ya siasa." Amesema Gates.

Makamo Rais wa China, Li Keqiang.
Makamo Rais wa China, Li Keqiang.Picha: dapd

Mwaka mmoja uliopita, China ilisitisha mahusiano yake ya kijeshi na Marekani, baada ya Marekani kuiuzia Taiwan silaha za kijeshi zenye thamani ya dola bilioni sita za Kimarekani. Pia iliifuta ziara ya Waziri Gates, iliyokuwa ifanyike mwaka huo.

Ziara hii ya Waziri Gates, inafanyika siku chache tu kabla ya ziara ya Rais wa China Hu Jintao, nchini Marekani, na wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, wizara zote mbili za ulinzi zingetaka kujenga taswira nzuri kabla ya viongozi wao wakuu kukutana.

Kwa miaka mingi, maafisa wa Marekani, akiwemo Waziri Gates mwenyewe, wamekuwa wakiitaka China ishiriki kwenye mdahalo wa moja kwa moja wa masuala ya makombora ya kujihami, silaha za nyuklia, na silaha na vita vya mtandao. Hata hivyo, China haijatoa kauli ya moja kwa moja ya kukubaliana na wazo hilo, japokuwa imekubaliana na wazo la kulifanyia uchunguzi eneo hilo.

Jenerali Liang amesema kwamba, mkuu wa utawala wa jeshi la China, Jenerali Chen Bingde, ataitembelea Marekani hivi karibuni na kwamba kuna mipango ya kuwepo ziara kama hiyo pia kutoka upande wa jeshi la Marekani.

Tayari Waziri Gates ameshakutana pia na Makamo Rais wa China, Xi Jinping, mtu ambaye anaangaliwa kama mrithi wa kiti cha urais, na ambaye mwaka jana aliteuliwa kuwa makamo mwenyekiti wa kamati kuu ya kijeshi, chombo cha juu cha kijeshi nchini humo.

Hapo kesho, Waziri Gates anatarajiwa kukutana na Rais Hu na Jumatano atatembelea makao makuu ya Kikosi cha Pili, ambayo ni kamandi maalum ya silaha za nyuklia na makombora ya China.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Josephat Charo