EU na Marekani zakutana .
8 Oktoba 2010Maafisa wa Umoja wa Ulaya wameahidi kuchukua hatua yenye ushirikiano zaidi kupambana na tishio la kigaidi wakati uzito wa tahadhari zilizotolewa na Marekani juma lililomalizika kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulio hayo barani Ulaya pindi ukithibitishwa.
Ahadi hiyo ilitolewa katika mkutano uliofanyika hapo jana huko Luxembourg kati ya Umoja huo na Marekani.
Naibu waziri wa usalama wa ndani kutoka nchini Marekani Jane Holl Lute, alialikwa kuhudhuria mkutano wa kawaida wa Umoja wa Ulaya wa mawaziri wake wa masuala ya ndani, mjini Luxembourg kulijadili suala la ushirikiano wao dhidi tishio hilo la usalama.
Afisa wa Umoja huo anayehusika na kupambana na ugaidi, Gilles De Kerchove aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano huo kuwa Lute amedhibitisha ukweli na uwepo wa tishio hilo la kigaidi bila ya kufafanua ni kipi hasa kilicholengwa katika tishio hilo.
Marekani ilitoa tahadhari hiyo baada ya kituo cha habari cha Fox kutoa taarifa kuwa kundi la kigaidi la Al Qaeda lilikuwa linapanga mashambulio ya ushirikiano katika maeneo makuu ya utalii mjini Paris Ufaransa, na Berlin Ujerumani, yaliyo mithili ya mashambulio ya Mumbai ya mwaka 2008 yaliosaabisha vifo vya watu 163.
Waziri wa ndani wa Ubeligiji, AnnemieTurtelboom,ambaye nchi yake ndiyo inayoshikilia urais wa kuzunguka wa Umoja huo wa Ulaya alizipa uzito mdogo mapendekezo kuwa hatua hiyo ya Marekani iliyojibiwa kwa dharura na Umoja huo wa Ulaya , ilizidishwa kuwa kubwa bure.
Turtelbloom alisema kuwa huo ni mtazamo wa Marekani na Umoja huo una mtizamo wake vilevile na kuwa Marekani ina jukumu la kisheria kutoa taarifa zote walizo nazo kwa raia wake.
Awali waziri wa ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere alisema kuwa hakuna haja ya kuzuwa mshtuko kuhusu taarifa hizo
Kufuatia kauli hiyo,waziri Turtelbloom alisisitiza haja ya Umoja huo wa Ulaya kushirikiana vyema zaidi katika kujibu matokeo kama haya.
Ameongeza kuwa wanachama wenzake wengi wa Umoja huo wamesisitiza haja ya kuwa na sauti moja hivyo serikali zilizo wanachama wa Umoja huo zinapaswa kuitahadharisha taasisi ya pamoja inayohusika namatukio,( SitCen ) kabla ya kutoa tahadhari kwa raia kuhusu tishio la kigaidi na vile vile kujaribu kuleta uwiano katika viwango vya tishio hilo .
Waziri Turtel Bloom alipendekeza kwamba maafisa wa wizara ya usalama wa ndani ya Marekani na mawaziri wa ndani wa Umoja huo wa Ulaya wakutane angalau mara moja kwa mwaka, na ameahidi pia ubadilishanaji wa taarifa zaidi katika eneo zima la bahari ya Atlantik kupitia mfumo wa rekodi za majina ya wasafiri (PNR) kwa abiria wanaosafiri kwa ndege, jambo linaloendelea kujadiliwa hivi sasa.
Mwandishi Maryam Abdalla
Mhariri: Abdul-Rahman