1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Kansela wa Ujerumani chashindwa uchaguzi wa Berlin

John Juma
13 Februari 2023

Chama cha kansela wa Ujerumani Olaf Scholz cha Social Democrat (SPD), kimepata pigo kubwa kwenye uchaguzi uliorudiwa jana katika jimbo la Berlin.

https://p.dw.com/p/4NPAy
Wiederholungswahl Berlin - CDU-Wahlparty
Picha: Odd ANDERSEN/AFP

Kwa mara ya kwanza katika miongo miwili, chama hicho kimeshika nambari ya pili baada ya chama cha upinzani CDU katika jimbo hilo. Chama cha Scholz kimekuwa kikishikilia kiti cha meya wa mji wa Berlin tangu mwaka 2001.

Hata hivyo bado haiko wazi iwapo mgombea wa  CDU  Kai Wegner ataongoza jimbo hilo la mji mkuu. Kutegemea matokeo ya mwisho, chama cha Kijani na SPD, vinaweza kuendeleza muungano wao wa sasa kwa kuungana na chama cha tatu.

Japo uchaguzi huo uliegemea zaidi masuala yanayowaathiri wakaazi wa jimbo hilo, kushindwa kwa chama cha Scholz kunajiri mnamo wakati kuna ukosoaji mkubwa dhidi yake, kuhusu kukawia kwake kutoa misaada ya kijeshi kwa Ukraine iliyovamiwa na Urusi mwaka uliopita. Mahakama ya kikatiba iliamuru uchaguzi wa jimbo hilo kurudiwa kwa kuwa haukushughulikiwa vyema mwaka 2021.