1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CDU chataka hatua kali dhidi ya uhamiaji Ujerumani

Iddi Ssessanga
11 Desemba 2023

Chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani, CDU kimezindua mpango wake wa kisera Jumatatu, kwa wito wa kufanya mabadiliko makubwa katika sera ya uombaji hifadhi ya Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/4a2lx
Ujerumani | KAtibu Mkuu wa CDU Carsten Linnemann
KAtibu Mkuu wa CDU Carsten Linnemann ametangaza rasimu ya mpango msingi wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Jumatatu, Desemba 11, 2023.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Rasimu ya programu kutokaCDU inataka Waislamu nchini Ujerumani kukumbatia maadili ya Ujerumani ambayo kwa kiasi kikubwa yanafuata misngi ya Kikristo, na kwamba wahamiaji lazima watambue haki ya kuwepo kwa taifa la Israel kama sehemu ya "utamaduni elekezi" wa Ujerumani (Leitkultur).

Rasimu hiyo ya programu ya CDU pia inataka Ujerumani irejee kutumia tena nishati ya nyuklia pamoja na kufanya mageuzi ya pensheni na soko la ajira.

"Wale wote wanaotaka kuishi hapa lazima watambue utamaduni wetu elekezi bila masharti," inasema rasimu hiyo. "Ni wale tu ambao wamejifunga kuheshimu utamaduni wetu elekezi ndiyo wanaweza kujumuika na kuwa raia wa Ujerumani."

Soma pia: Wulff atoa wito wa uvumilivu wa kidini

Katibu Mkuu wa CDU Carsten Linnemann aliielezea rasimu ya mpango-msingi huo kama hati elekezi ya kutayarisha chama kwa ajili ya uchaguzi ujao wa nchi nzima, unaotazamiwa kufanyika 2025.

Ujerumani | Mwenyekiti wa CDU Friedrich Merz
Mwenyekiti wa CDU Friedrich Merz katika mkutano wa chama ndugu na CDU, CSU kinachotawala jimbo la Bavaria.Picha: Peter Kneffel/dpa/picture alliance

"Kama kutaitishwa uchaguzi mkuu wa mapema, tutakuwa tayari," alisema Linnemann, wakati akiwasilisha rasimu ya kwanza mjini Berlin. Watu nchini Ujerumani wanahisi kutokuwa salama na wanahitaji mwelekeo na msaada, alisema Linnemann. ""Na tutatoa mwelekeo huu kupitia mpango huu wa kisera.

Uislamu hautakuwa tena 'sehemu ya Ujerumani'

Rasimu ya mpango huo inakitenganisha chama na matamshi ya rais wa zamani wa Ujerumani Christian Wulff, mwanachama wa CDU ambaye alitangaza mwaka wa 2010 kwamba "Uislamu sasa pia ni sehemu ya Ujerumani."

Badala yake, rasimu ya programu inasema kwamba "Waislamu ambao wanashiriki maadili yetu ni sehemu ya Ujerumani."

Kuhusu uhamiaji, rasimu ya mpango wa CDU inataka kila mhamiaji anayeomba hifadhi katika Umoja wa Ulaya apelekwe "nchi ya tatu salama" ambapo maombi yatazingatiwa, na kuweka viwango vya hiari vya idadi ya wakimbizi ambao kila nchi ya Umoja wa Ulaya itakubali.

"Muungano wa hiari" kutoka miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya unaweza kujitolea kupokea baadhi ya wakimbizi kila mwaka - lakini hadi kiasi fulani tu, kulingana na rasimu hiyo. Chama hicho hakikubainisha ni watu wangapi ambao CDU itakuwa tayari kupokea kwa ajili ya hifadhi nchini Ujerumani kila mwaka.

Ujerumani, Berlin | Angela Merkel
Chama cha CDU kilipoteza madaraka baada ya kuondoka kwa Kansela Angela Merkel kufuatia uchaguzi wa 2021.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waraka huo wenye kurasa 70 umepewa kichwa cha habari "Kuishi katika Uhuru: Kuiongoza Ujerumani kwa Usalama katika Wakati Ujao." Rasimu hiyo imewasilishwa kwa kamati za ngazi za juu za chama cha CDU na inatazamiwa kupitishwa rasmi na bodi kuu ya chama katika mkutano wa faragha katikati ya mwezi wa Januari.

Soma pia: Merkel awaomba wanasiasa kuweka pembeni tofauti zao

Kisha itajadiliwa na wanachama na kupitishwa na wajumbe 1,001 wa CDU katika mkutano wa chama mwezi Mei.

Chama cha CDU, cha kansela wa zamani Angela Merkel, kilizindua mchakato wa kuandaa mpango mpya wa sera ya msingi baada ya kupoteza madaraka katika uchaguzi wa bunge wa 2021 uliomweka madarakani Kansela Olaf Scholz.

Mpango wa msingi wa sasa wa chama hicho  uliandaliwa mwaka 2007.