1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bundesliga-B.Munich yaumana na Stuttgart

Mabingwa wa Ujerumani B.munich waweza kuambiwa buriani leo ikiwa watashindwa kuwika mbele ya Stuttgart katika mpambano wa kufa-kupona.Kesho ni zamu tena ya London marathon na mabingwa wawili Tergat (Kenya) na Gebreselassie (Ethiopia) wana miadi .

Stuttgart ilipoizaba Wolfsburg juzi bao 1:0

Stuttgart ilipoizaba Wolfsburg juzi bao 1:0

Manchester United ikijaribu leo kupanua tena mwanya wake hadi point 6 kutoka mahasimu wao Chelsea . kinyan’ganyiro cha kombe la klabu bingwa barani Afrika baada ya Al Ahly kutamba nyumbani dhidi ya mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Katika bundesliga-Ligi ya Ujerumani mpambano leo ni kati ya mabingwa Bayern Munich na Stuttgart iliopo nafasi ya 3 ya ngazi ya Ligi. Huu ni mpambano wa kufa kupona kwa Bayern Munich,kwani baada ya kupigwa kumbo na AC Milan katika champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya na Schalke ikiongoza orodha ya Ligi nyumbani,Munich lazima iishinde Stuttgart jioni hii ili alao kuipokonya nafasi ya 3 na kuweka matumaini ya kucheza champions League msimu ujao.Munich iko pointi 6 nyuma ya viongozi wa Ligi Schalke , pointi 4 nyuma ya Werder Bremen iliopo nafasi ya pili na pointi 2 nyuma ya mahasimu wao wa jioni hii Stuttgart.

Kipa wa Bayern munich Oliver kahn kabla timu hizi mbili kuingia uwanjani alinukuliwa kusema, “Mechi hii ni nafasi kubwa kwetu kunyakua nafasi ya 3 katika ngazi ya Ligi…Ni finali ya kwanza kati ya 5 zinazotukabili.Sote tunaelewa ni muhimu sana kwa Bayern munich kucheza champions League.”

Stuttgart kati ya wiki hii ilikata tiketi ya finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani kwa kuikomea Wolfsburg bao 1:0 na imeweka miadi mjini Berlin mwezi ujao na Nüremberg.

Stuttgart isitoshe, inacheza nyumbani na binafsi inaania tiketi ya kucheza msimu ujao wa champions League.Munich, ikilazwa leo na Stuttgart itajikuta pointi 9 nyuma ya viongozi Schalke endapo Schalke ikiilaza Cottbus huko Gelsenkirchen.Lakini ushindi huko Stuttgart kutaongeza nafasi za kunyatia tena taji la ubingwa .Munich imetamba mbele ya Stuttgart katika mapambano 9 kati ya 12.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza,Manchester imepania jumamosi hii kufungua upya mwanya wa pointi 6 kileleni kati yake na Chelsea baada ya Chelsea kuuziba mwanya huo kati ya wiki hadi pointi 3.Manchester ilifungua mwanyawa pointi 6 jumaane walipoikomea Shefield United mabao 2:0 lakini mwanya huo ukapunguzwa tena hadi pointi 3 pale Chelsea ilipoibomoa West ham United kwa mabao 4-1 siku moja baadae.Jioni hii basi ushindi dhidi ya Middlesbrough utawarudishia uongozi huo wa pointi 6 kileleni mwa premier League.

Katika ligi ya Spain,Ronaldinho,stadi wa Brazil arudi kesho uwanjani kujiunga na mastadi 2 wenzake Eto wa Kamerun na Messi wa Argentina ili kuirejesha Barcelona kileleni mwa La Liga.Ronaldinho alikosa kucheza mechi 2 zilizopita baada ya kuumwa na homa ya mafua . Habari za kurejea kesho uwanjani kwa Ronaldinho bila shaka hazikuwafurahisha mahasimu wao Villarreal.

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la klabu bingwa la Amerika kusini-Libertadores Cup-mabingwa watetezi Internacional walianushwa katika changamoto ya kwanza kabisa ya kinyan’ganyiro hiki walipopigwa kumbo licha ya kuilaza Nacional bao 1:0.Nacional mojawapo ya klabu maarufu za Uruguay na mabingwa mara 3 wa zamani wa kombe hilo,wamekata tiketi ya duru ijayo wakija nyuma ya Sarsfield ya Argentina.

Hatima ya Young Africans ya Tanzania katika kombe la klabu bingwa inakatwa huko Mwanza jumamolsi jioni ambako inabidi kuingia uwanjani kufuta madhambi ya mabao 3:0 waliofanya duru iliopita huko Tunisia.Esperence mahasimu wao wakijulikana wana ngome imara ,walipania tangu nyumbani kutoiruhusu Yanga kuwatilia kitumbua choa mchanga huko Mwanza,hata ikiwa Yanga wanacheza nyumbani.

Mpambano huu tangu awali ulikuwa mgumu kwa yanga kama alivyoeleza mwanamichezo wetu George Njogopa:

Duru hii ya tatu ilifunguliwa ijumaa na changamoto kati ya mabingwa Al Ahly ya Misri huko Cairo na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini katika kile baadhi ya mashabiki walikiona marudio ya finali ya kombe hili ya mwaka 2001.

Etoile du Sahel pia ya Tunisia kama Esperence, imebakia nyumbani kucheza na Marantha Fiokpo ya Togo.Al-Ittihad ya Libya inacheza na Etoile wakati mjini Casablanca ,Waydad ya jiji hilo inaikaribisha ASEC Abidjan ya Ivory Coast.

Ama katika duru ya tatu ya kinyan’ganyiro cha kombe la shirikisho la Afrika CAF- Gafsa ya Tunisia inaikaribisha leo ATRACO ya Rwanda.Timu hizi 2 ziliagana kwa mabao 2-2 mjini Kigali duru iliopita.

AL Merrreikh ya Sudan iko nyumbani kuumana na ASO CHLEF yageria.Green Buffaloes ya Zambia inacheza leo na Ismailia ya Misri wakati Astres Douala ya Kamerun, inakumbana na Benefica Luanda ya Angola.

Mjini Harare Mwana Africa ya Zimbabwe ilipangwa kuonana na Etoile Filante ya Burundi ilioshinda nyumbani duru ya kwanza kwa mabao 2:0.

Tayari kati ya wiki hii, Kwara United ya Nigeria iliitoa Union Douala ya Kamerun kupitia mkwaju wa penalty wa kutatanisha uliozusha balaa la mashabiki na kupigwa kwa rifu kutoka Gambia.Kwara ilishinda kwa mabao 3-2.

RIADHA:

Kesho –asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano katika barabara za jiji la London jumapili:Majogoo wa wili wa mbio za masafa marefu waliopamabana sana katika Olimpik-bingwa wa rekodi ya dunia wa mbio za marathon mkenya Paul Tergat na bingwa wa rekodi kadhaa za masafa marefu-pamoja na mita 5000 na 10.000 Haile Gebreselassie wa Ethiopia wanakutana katika London marathon:

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mabingwa hawa 2 kukutana uso kwa uso katika mbio za marathon tangu 2002 pale Tergat alipokomesha mlolongo wa ushindi 12 wa Selassie mjini London.Lakini ushindi hasa mara ile ulimwendea Khalid Khannouchi wa Marekani huko Gebreselassie akibidi kuridhika na nafasi ya 3 nyuma ya Tergat.Lakini zile zilikuwa mbio zake za kwanza za marathon.Kinyume na hapo kesho.

Tergat lakini, ndie bingwa wa rekodi ya dunia .Marathon ni tofauti na mbio za uwanjani ambamo mnamo miaka ya 1990 tangu katika olimpik hata nje yake, mkenya Paul Tergat alikuwa nambari 2 tu kwa Haile Gebreselassie.Sasa akiwa na rekodi ya dunia alioiweka Berlin,Septemba mwaka juzi,Paul Tergat anatamba na mshindi kati yao kesho huenda akatoroka na kitita cha dala robo-milioni.

Mbio za marathon kwa wanawake pia zinazozusha changamoto kali zkiingiza muethiopia Berhane Adere,Gete Wami wakipambana na wachina Zhou Chunxiu-bingwa wa Asia.

 • Tarehe 20.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHcJ
 • Tarehe 20.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHcJ