1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boris Johnson: Shujaa wa Brexit anaezongwa na 'partygate'

Iddi Ssessanga
19 Januari 2022

Kwa muda mrefu Boris Johnson amekuwa akipuuza ukweli, lakini utayari wa waziri mkuu huyo wa Uingereza kukabili hatari zaidi kuliko watu wengine ulikuwa muhimu katika ushindi mkubwa wa chama chake kwenye uchaguzi wa 2019.

https://p.dw.com/p/45mzm
London Rede Boris Johnson im Unterhaus
Picha: PRU/AFP

Kwa wakosoaji wake wengi, ukweli umeanza hatimaye kumtia kitanzi mwanasiasa ambaye wakati mmoja alielezewa na waziri mkuu wa zamani David Cameron kama "nguruwe aliyepakwa mafuta" kutokana na uwezo wake wa kukwepa mikwaruzo ya kisiasa.

Johnson alikuwa amekabiliana vilivyo na madai ya kusema uongo hapo awali, lakini hivi sasa anapata wakati mgumu zaidi kupandisha mabega juu ya madai kwamba wafanyakazi wake wa Downing Street walikuwa wakijishughulisha na hafla wakati nchi nzima ikivumilia chini ya vikwazo vya kukabiliana na janga la Covid.

Kiwango cha vifo kutokana na virusi vya Corona nchini Uigereza ni cha pili, ikitanguliwa tu na Urusi barani Ulaya, na Johnson mwenyewe aliponea chupu chupu kufa katika janga hilo.

England Premierminister Boris Johnson
Boris Johnson akichanjwa dhidi ya virusi vya Corona. Waziri Mkuu aliwahi kuugua Covid-19 hadi kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.Picha: Simon Dawson/Avalon/Photoshot/picture alliance

Ameweka matumani juu ya kampeni kubwa ya chanjo kuchanja bahati yake ya kisiasa, lakini ufichuzi unaozidi juu ya kashfa ya "partygate" umepekelea kushuka kwa umaarufu wa chama cha Kifahidhina, huku miito ikiongezeka ya kumtaka ajiuzulu.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikaidi wito wa kujiuzulu

Johnson, mwenye umri wa miaka 57, alichukuwa uongozi wa chama cha Conservative na uwaziri mkuu Julai 2019, na kujiimarisha madarakani miezi sita baadaye kwa ushindi mkubwa wa uchaguzi kwa ahadi ya kufanikisha mchakato wa kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, na kwamba Waingereza wangeanza kufurahia matunda ya hatua hiyo.

Ahadi za Brexit zisizotimia

Lakini licha ya kukubali makubaliano ya biashara na Brussels, kuondoka katika kanda hiyo -- na kukomesha uhuru wa kuingia nchini humo kwa watu na wafanyakazi -- kumeshuhudiwa vurugu na kuchochewa na janga la Covid-19.

Wakati huo huo, wakati bei za nishati zikipanda na mfumuko wa bei ukiongezeka, Johnson anakabiliwa na upinzani baada ya kuvunja ahadi yake ya uchaguzi kwa kutangaza kupandishwa kwa kodi ili kujaza mapengo ya nakisi ya bajeti katika sekta ya afya na huduma za kijamii.

Soma pia: Uingereza yaondoka rasmi Umoja wa Ulaya

Lakini waziri mkuu huyo, anaewahusudu sana watangulizi wa kihafidhina kama vile Winston Churchill na Margaret Thatcher, bado anasisitiza kuwa "anainua" fursa za kiuchumi kote nchini Uingereza.

England | Premierminister Boris Johnson und Queen Elizabeth
Johnson akiwa na Malikia wa Uingereza, Elizabeth wa Pili.Picha: Dominic Lipinski/AFP/Getty Images

Huku baadhi ndani ya chama chake wakiwa na hofu kuhusu wa serikali za miji na majiji unaotarajiwa mwezi Mei, Johnson anaweka dau lake kwamba hulka yake chanya na viapo vya mustakabali wa furaha na ustawi, bado vinavuma miongoni mwa wapigakura wengi.

Lakini kwa idadi inayoongezeka, hasi za Johnson zinamfanya kutokuwa mtu anayefaa kushika tena wadhifa huo, na ana msururu mrefu wa matamshi tata yaliyochapishwa akiwashambulia wanawake, mashoga, watu weusi na Waislamu.

Mfalme wa dunia

Alexander Boris de Pfeffel Johnson alizaliwa mjini New York mwaka 1964. Dada yake alisema kwamba akiwa mtoto, alipenda kuwa "mfalme wa dunia."

Alitumia sehemu ya utoto wake katika mji mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Brussels, ambapo baba yake Stanley alifanya kazi katika Tume ya Ulaya. Kisha alihudhuria shule ya watu wa tabaka la juu ya Eton huko Uingereza kabla ya kusoma Kigiriki na Kilatini katika Chuo Kikuu cha Oxford.

Katika wasifu wake "Boris Johnson: The Gambler", mwandishi wa habari Tom Bower anaelezea ufuataji wanawake wa mfululizo uliopelekea kuvunjika kwa ndoa mbili za kwanza za Johnson na uhusiano wake tulivu na ukweli.

Soma pia: Waziri mkuu Boris Johnson akabiliwa na wakati mgumu

Johnson anaaminika kuwa na watoto saba, wakiwemo wawili aliowazaa na mke wake wa tatu Carrie, 33, ambaye alijifungua mtoto wa kike mwezi uliopita.

England | Trauer um Captain Sir Tom Moore
Johnson na mke wa sasa Carrie Symonds wakiwa nje ya ofisi ya waziri mkuu mtaa wa Downing 10.Picha: John Sibley/REUTERS

Alifanya kazi kwa mara ya kwanza kama mwandishi wa habari wa The Times, ambapo alifutwa kazi kwa kubuni nukuu, na akahamia kuwa mwandishi wa Brussels wa gazeti la Daily Telegraph.

Hapo alijipatia jina kwa kuandika "Euro-myths" -- madai yaliyotiwa chumvi kuhusu Umoja wa Ulaya, kama vile mipango inayodaiwa ya kusawazisha ukubwa wa mipira ya kondomu na ndizi.

Mwisho wa safari?

Johnson kisha aliingia katika siasa lakini, mwaka wa 2004, aliondolewa kwenye baraza la mawaziri kivuli la chama cha Conservative kwa kudanganya kuhusu uhusiano wa nje ya ndoa.

Soma pia: Uhaba wa mafuta Uingereza waathiri huduma muhimu kama uuguzi

Alijitosa kuwa meya wa jiji la London lenye historia ya kukichagua chama cha Labour, na ambao unaelemea sana Ulaya mnamo mwaka 2008, mafanikio ambayo wadadisi wanasema yalitokana na ujasiri wake wa kukataa kuheshimu maagano.

Johnson alihisi kuchanganyikiwa kuhusu njia ya kushika katika kura ya maoni ya Brexit ya 2016, akitayarisha orodha ya faida na hasara za uanachama wa Umoja wa Ulaya, kabla ya kuweka nguvu yake ya kisiasa nyuma ya kampeni ya "kuondoka".

Umaarufu wake, na mwelekeo wa kutia chumvi, ulisaidia kupiga kampeni, na aliingilia kati mnamo 2019 kumaliza mdororo wa kisiasa uliofuata kwa kuchukua udhibiti wa chama cha Kihafidhina kutoka kwa Theresa May.

Dominic Cummings sagt vor Mitgliedern von Unterhaus-Ausschüssen des britischen Parlaments aus
Aliekuwa msaidizi Mkuu wa Johnson, Dominic Cummings, amesema yuko tayari kula kiapo kutoa ushahidi dhidi ya Johnson, hatua inayoweza kummaliza kabisaa waziri mkuu huyo.Picha: Matt Dunham/AP/picture-alliance

Ndani ya miezi sita, Johnson alikuwa amejadili tena mkataba wa May wa Brexit uliokosolewa sana, akashinda uchaguzi na kuitoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya.

Soma pia:Maoni: Urithi wenye sumu wa Brexit anaoacha Theresa May 

"Wale ambao hawakumchukulia kwa uzito walikosea," Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema wakati huo. Lakini aliwashutumu watetezi wa Brexit kwa kusema "uongo na kutoa ahadi za uongo".

Msaidizi mkuu wa zamani wa Johnson Dominic Cummings sasa amekuwa akivujisha taarifa dhidi yake, ikiwemo juu ya marekebisho ya gharama ya juu ya gorofa yake ya Downing Street.

Cummings anasema yuko tayari kuapa kwamba Johnson "alilidanganya bunge kuhusu hafla", madai ambayo iwapo yatakuwa na ukweli, yanaweza kuwa msumari wa mwisho katika jeneza, hata kwa mwanasiasa mwenye kipaji chake cha ukwepaji. Johnson amekanusha madai hayo.

Chanzo: AFPE