1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi wa kishindo wa wahafidhina Uingereza

Oumilkheir Hamidou
13 Desemba 2019

Chama cha kihafidhina cha waziri mkuu Boris Johnson kimeshinda kwa wingi mkubwa uchaguzi mkuu Uingereza. Umoja wa Ulaya wametoa pongezi zao na kuhimiza mchakato wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya uidhinishwe haraka.

https://p.dw.com/p/3UjoC
Großbritannien Boris Johnson nach der Wahl 2019
Picha: Reuters/T. Mukoya

"Serikali ya kihafidhina ya nchi hii imepatiwa madaraka makubwa zaidi ya kukamilisha mchakato wa Brexit. Na sio tu kukamilisha mchakato wa Brexit bali pia kuiunganisha nchi yetu na kutanguliza mbele mahitaji muhimu ya Waingereza."

Amesema hayo waziri mkuu Boris Johnson mara baada ya kuthibitika ushindi wa chama chake cha kihafidhina Tories. Boris Johnson amepania anasema kuitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya hadi ifikapo january 31 mwaka 2020. Amewashukuru wote wale waliokipigia kura kwa mara ya kwanza chama cha kihafidhina na kukisaidia chama chake kujipatia wingi mkubwa wa viti bungeni."Mmetupatia kura zenu bila ya kujali kuwa nyie si wahafidhina" amesema Boris Johnson baada ya idadi  isiyo ndogo ya wafuasi wa chama cha upinzani cha Labour kukipigia kura chama hicho cha kihafidhina.

Mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani, Jeremy Corbyn amesema hatogombea tena wadhifa huo kufuatia pigo la uchaguzi mkuu wa jana.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto) na rais wa Marekani Donald Trump
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kushoto) na rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

 Uingereza na Marekani wako huru kufikia makubaliano mepya ya biashara

Pongezi kwa ushindi wa chama cha kihafidhina zimetumwa na viongozi kadhaa wa dunia. Rais wa Marekani Donald Trump anasema katika salam zake za pongezi ushindi wa Johnson unamaanisha Uingereza na Marekani zitakuwa huru "kufikia makubaliano mepya ya biashara baada ya Brexit."

Viongozi wa Umoja wa ulaya wameupongeza pia ushindi wa Boris Johnnson na kutoa wito wa kupigiwa kura haraka na bunge la nchi hiyo mchakato wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya. Hata hivyo waziri mkuu wa jamhuri ya Cheki anaonya ushindi wa Boris Johnson "ni habari mbaya kwa ulaya."Ameshinda na sasa  kwa bahati mbaya watatoka" amesema waziri mkuu Andrej Babis.

Mwenyekiti wa baraza la Ulaya Charles Michel amempongeza kwa upande wake Boris Johnson na kusema Umoja wa ulaya uko tayari kujadiliana kuhusu makubaliano ya biashara huru lakini amekwepa kusema kama makubaliano hayo yanaweza kufikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.