1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Yair wakubaliana kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran

14 Julai 2022

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid wanatarajiwa kusaini ahadi ya pamoja ya kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/4E6yT
Israel | Joe Biden in Jerusalem
Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

 

Taarifa za kusainiwa kwa ahadi hiyo zimekuja mnamo siku ya pili ya ziara ya Rais Joe Biden nchini Israel, ambayo pia itamfikisha nchini Saudi Arabia.

Akizungumza na televisheni ya Israel mjini Jerusalem, Biden amesema anaunga mkono uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran, kama chaguo la mwisho.

Kauli yake hiyo inachukuliwa kama kuridhia wito wa Israel kuyataka mataifa yenye nguvu duniani kuifanya Iran ijue bayana kuwa inakabiliwa na kitisho dhahiri cha kivita.

Soma pia:Mazungumzo ya mkataba wa nyuklia na Iran mbioni kuanza tena

Hata hivyo, Rais huyo wa Marekani ameshikilia msimamo wa utawala wake wa kutaka kufufua makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, mchakato unaopingwa vikali na Israel.

Mtangulizi wa Biden, Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya mwaka 2015, uamuzi ambao Biden amesema haukuwa wa busara.

''Nadhani lilikuwa kosa kubwa sana kwa rais wa zamani kujiondoa katika makubaliano yale." Alisema Biden na kuongeza  Iran iko karibu zaidi kupata silaha za nyuklia kuliko wakati mwingine.

"Haihusiani na ikiwa kikosi cha walinzi wa mapinduzi kitaendelea na shughuli zake au la" alisema na kusisitiza kuwa hilo lunaweza kulishughulikiwa wakati huo huo kukawa na makubaliano ya kuudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran.

Kikosi maalum cha Iran katika orodha ya magaidi Marekani

Walinzi wa mapinduzi ni kikosi maalumu katika jeshi la Iran, ambacho Marekani imekiweka kwenye orodha ya magaidi, Biden amesema hatakubali shinikizo la Iran kukiondoa kwenye orodha hiyo, hata kama hilo linamaanisha kutofikiwa kwa makubaliano mapya.

Israel | Joe Biden in Jerusalem
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa nchini IsraelPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Hadi sasa Iran haijasema chochote juu ya ahadi hiyo ya pamoja ya Marekani na Israel inayosainiwa mjini Jerusalem.

Hapo jana Ikulu ya mjini Tehran ilisema katika tangazo lake, kuwa juhudi zote za Marekani kuitafutia amani Israel katika mashariki ya kati, zitaambulia patupu.

Soma pia:Iran yaondoa kamera za IAEA kwenye vinu vyake

Rais Biden anatarajiwa hapo kesho kuitembelea Saudi Arabia, akiazimia kutaka ushirikiano wa taifa hilo la kifalme katika kushusha bei ya mafuta, suala ambalo linamkosesha usingizi katika siasa za nyumba.

Lakini pia atakuwa na lengo la kuhimiza maelewano kati ya nchi hiyo ya ghuba na Israel, katika mwendelezo wa sera ya Marekani ya kutaka Israel ikubaliwe na kuchukuliwa kama jamii ya kawaida katika ukanda mpana wa mashariki ya kati.

Marekani yaanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran