1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaonywa dhidi ya kuhujumu mazungumzo ya Nyuklia Vienna

Saumu Mwasimba
12 Machi 2022

Uingereza,Ufaransa na Ujerumani zimetahadharisha dhidi ya hatua za kutumia vibaya mazungumzo ya Nyuklia ya Iran

https://p.dw.com/p/48OXN
Österreich | Atomgespräche mit dem Iran
Picha: EU Delegation in Vienna/Handout/AFP

Uingereza,Ufaransa na Ujerumani zimetahadharisha dhidi ya hatua za kutumia vibaya mazungumzo ya Nyuklia ya Iran yanayofanyika huko Vienna. Onyo hili limeelekezwa kwa Urusi ambayo inatuhumiwa kuchelewesha hatua ya kufikiwa makubaliano ili ivute muda wa kupata mafanikio katika uvamizi wake nchini Ukraine.

Wajumbe kwenye mazungumzo ya Vienna siku ya Ijumaa waliyasimamisha mazungumzo hayo licha ya kufikia hatua ya kukaribia kupata makubaliano ya kufufua mkataba wa Nyuklia wa mwaka 2015 uliofikiwa na nchi hiyo ya Iran na nchi .zenye nguvu duniani.

Wien | Iran Nuklearabkommen
Picha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Lengo kubwa la makubaliano hayo ni kudhibiti shughuli za Kinyuklia za Iran.

Hata hivyo hujuma hizi zinazotokea kwenye mazungumzo hayo zimekuja baada ya Urusi kusema inataka kupata hakikisho la nchi za Magharibi kwamba vikwazo vya kiuchumi ilivyoiwekea nchi hiyo kufuatia mgogoro wake na Ukraine havitoathiri shughuli zake za kibiashara na Iran.

Taarifa iliyotolewa Jumamosi na wajumbe mjini Vienna  imeeleza kwamba hakuna mtu yoyote anayepaswa kuyatumia majadiliano kuhusu rasimu ya JCPOA kujipatia hakikisho la aina yoyote ambalo liko nje ya rasimu au mkataba huo.

Taarifa hiyo ni ya mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza,Ufaransa na Ujerumani ambazo ni pande tatu za Ulaya zinazoshiriki mazungumzo ya Vienna.

Österreich Wien | Internationale Atomenergie-Organisation | Rafael Mariano Grossi
Picha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Taarifa hiyo pia imebaini kwamba kitendo hicho kinaweza kuyaweka hatarini makubaliano hayo ya mpango wa Nyuklia wa Iran kuvunjika na kuwanyima wananchi wa Iran nafasi ya kuondolewa  vikwazo na kwa upande mwingine pia kuinyima nafasi jumuiya ya kimataifa kupata hakikisho wanalolihitaji kuhusu mpango huo wa Nyuklia wa Iran. Duru hii ya sasa ya mazungumzo ilianza mwishoni mwa mwezi Novemba katika mji mkuu wa Austria,Vienna,yakiwashirikisha Uingereza,Ufaransa,China,Ujerumani.

Iran na Urusi na Marekani ikishiriki sio moja kwa moja.Baada ya mazungumzo hayo kusimama Ijumaa Marekani imeutupa mpira kwa Iran na Urusi kuamua hatma.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Sudi Mnette