1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Merkel anatumai hatua zaidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa

10 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKU

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema leo hii kwamba ana matumaini ya kufanikisha hatua nyengine katika mwelekeo sahihi kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa mkutano wa Viongozi wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo makubwa ya viwanda duniani utaofanyika mwezi wa Juni nchini Ujerumani baada ya kuuongoza Umoja wa Ulaya katika kuweka hatua kadhaa za kupambana na tatizo hilo.

Merkel ambaye nchi yake inashikilia Urais wa Umoja wa Ulaya na ule wa Kundi la Mataifa Manane alitowa wito kabla ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya kutaka Ulaya iweke mfano kwa wengine kama vile Marekani na China katika kupambana na ongezeko la hali ya ujoto duniani. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira kwa angalau asilimia 20 kutoka viwango vya miaka ya 1990 katika kipindi cha miaka 13 ijayo.

Amesema kwa jambo hilo Ulaya ina dhima kuu na wanaamini kwamba wanaweza pia kuzalisha ajira zaidi na fursa za kusafirisha nje bidhaa kwa watu walioko barani humo kwa kupitia ubunifu zaidi kwenye fani za matumizi ya nishati zinazoweza kutumia upya.