1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya standard Chartered yaridhia kulipa faini

MjahidA15 Agosti 2012

Benki ya Uingereza ya Standard Chartered imetangaza kulipa faini ya euro millioni 340 ilioagizwa na taasisi ya Marekani inayochunguza mabenki

https://p.dw.com/p/15prz
Benki ya Standard Chartered
Benki ya Standard CharteredPicha: Kin Cheung/AP/dapd

Benki hiyo inadaiwa kuwasaidia wateja wake, raia wa Iran, kukwepa vikwazo vya Marekani. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya tuhuma kuwa Benki hiyo ilificha biashara takriban 60,000 iliokuwa ikifanya na wateja hao wa Iran iliogarimu dola bilioni 250 kwa kipindi cha miaka kumi.

Hatua hii ya kulipa faini ya euro millioni 340 haikutarajiwa na benki hiyo badala yake walidhani kuwa huenda wakafutiwa leseni ya kufanya kazi. Wateja hao ni Benki kuu ya Iran inayoungwa mkono na serikali na pamoja na benki ya taifa ya Iran ambazo zote mbili zimeshutumiwa na Marekani kwa kuisaidia Tehran kujipatia silaha za nyuklia na pia kufadhili shughuli za ugaidi.

Katika mkataba wa maelewano kati ya benki ya Standard Chartered na wizara ya fedha ya Marekani, ni kwamba benki hiyo imekubali shirika la kushughulikia uporaji wa fedha kuwepo katika benki hiyo tawi la New York kwa muda wa miaka miwili, na pia kuteua wakakaguzi wa ndani kuangalia ushirikiano wao kwa vikwazo vya Marekani.

Shirika la nguvu za atomiki la Iran
Shirika la nguvu za atomiki la IranPicha: picture-alliance/dpa

Mkurugenzi mkuu wa Standard Chartered, Peter Sands, alikuwa Marekani wakati mpango huo ulipoafikiwa. Hata hivyo, idara ya fedha jijini New York imezua maswali iwapo benki hiyo inapaswa kupokonywa leseni na kutofanya kazi tena nchini Marekani.

Kulingana na mchambuzi nchini humo, Erin Davis, faini iliokubali kutoa banki hiyo ya euro millioni 340 sio kubwa sana na haitakuwa na madhara yoyote kifedha katika benki hiyo kwa sababu hivi majuzi waliripoti kupata faida ya euro bilioni 3.95

Hapo jana wizara ya fedha ilisema japokuwa makubaliano yameafikiwa kwa benki hiyo kulipa faini, bado uchunguzi wake utaendelea kuhakikisha kuwa Standard Chartered inalipa vilivyo kutokana na makosa walioyafanya.

Huku hayo yakiarifiwa shirika la muungano dhidi ya silaha za nyuklia za Iran limesema katika taarifa yake kwamba shirika lolote la fedha ambalo litapatikana kuhujumu vikwazo vilivyowekewa Iran linapaswa kufutiwa leseni yake na kutokubaliwa tena kufanya kazi nchini Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard Membe
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Bernard MembePicha: AP Photo

Katika muongo uliopita Marekani pamoja na washirika wake waliviimarisha vikwazo dhidi ya benki za Iran, taasisi na watu binafsi kwa nia ya kusimamisha mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia za Iran.

Huku hayo yakiarifiwa Jana wabunge wa Marekani waliihimiza serikali yao kuchukua hatua dhidi ya Tuvalu na Tanzania, nchi zilizoshutumiwa kuhujumu vikwazo vilivyowekwa na Marekani kwa Iran, baada ya nchi hizo kuweka bendera zao katika meli za Iran.

Hata hivyo, mapema wiki hii serikali ya Tanzania imesema kuwa hatua ya kuweka bendera yake kwa meli 36 za Iran ilichukuliwa na wakala wake nchini Dubai bila ya Tanzania kufahamishwa au kuridhia. Lakini kupitia waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernad Membe ni kwamba zitawafutia usajili meli hizo 36

Tuvalu nayo imekiri kuwa imeipa usajili kampuni ya meli za Iran lakini imesema itafuatilia na kuchukua hatua kwa kila meli ya Iran itakayokuwa inapeperusha bendera ya Tuvalu

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri Othman Miraji