Ben Ali na mkewe waadhibiwa miaka 35
21 Juni 2011Hukumu hiyo imetolewa wakati akiwa Saudi Arabia alikokimbilia, tangu miezi sita iliyopita, kufuatia mapinduzi yaliyochochea vuguvugu la kidemokrasia katika ulimwengu wa Kiarabu. Katika kesi iliyosikilizwa siku moja, rais wa zamani wa Tunisia, Ben Ali amekutikana na hatia ya wizi na kumiliki vyombo vya dhahabu,almasi na vito vingine vya thamani pamoja na mamilioni ya fedha taslimu kinyume na sheria. Hata mkewe Leila Trabelsi aliejulikana kwa maisha yake ya fahari, amepewa kifungo cha miaka 35. Jaji Touhami Hafi aliesoma hukumu ya adhabu hiyo mahakamani katika mji mkuu Tunis alisema kuwa Ben Ali na mkewe watapaswa kulipa faini ya dola milioni 65.6 vile vile.
Ben Ali adai mashtaka ni njama ya kisiasa
Kwa mujibu wa ripota mmoja wa shirika la habari la Reuters aliekuwepo mahakamani, hukumu juu ya mashtaka mengine ya kudhibiti madawa ya kulevya na silaha itatolewa Juni 30. Katika taarifa iliyotolewa mapema hiyo jana na mawakili wanaomtetea Ben Ali, rais huyo wa zamani alisema kwamba silaha anazotuhumiwa kudhibiti kinyume na sheria, zilikuwa zawadi kutoka viongozi wa kimataifa; na vito vya thamani, ni zawadi zilizotolewa na wanadiplomasia wa kigeni kwa mke wake Leila. Amesema, fedha taslimu na madawa, yalipelekwa nyumbani kwake na katika makao rasmi ya rais, baada ya yeye kuondoka nchini humo. Amesema, hiyo ilikuwa njama dhidi yake. Ben Ali, amekanusha mashtaka yote dhidi yake. Akaongezea kuwa yeye ni mhanga wa njama ya kisiasa na kwamba alifanyiwa ujanja kuondoka Tunisia.
Kesi ya Ben Ali imefuatilizwa kwa makini Misri
Ben Ali , mkewe na watoto wao walikimbilia Saudi Arabia Januari 14 mwaka huu, baada ya kushinikzwa na maandamano makubwa ya kupinga utawala wake wa miaka 23 nchini Tunisia. Wakati wa utawala huo, Ben Ali, familia yake na ya mkewe zilijirundikia mali; na wale waliothubutu kumpinga, walikamatwa na vikosi vya usalama. Mapinduzi ya Tunisia yaliwasisimua mamilioni ya watu katika ulimwengu wa Kiarabu, wakiwa na matatizo yale yale ya ukosefu mkubwa wa ajira, ughali wa maisha na serikali za ukandamizaji. Kesi ya Ben Ali imefuatilizwa kwa makini nchini Misri, ambako rais wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak, anatazamiwa pia kupandishwa kizimbani kwa mashtaka ya mauaji ya waandamanaji.
Mwandishi: Martin,Prema/rtre
Mhariri:Abdul-Rahman