Bashir asema Abyei ni sehemu ya Sudan Kaskazini
25 Mei 2011Rais Bashir ametoa kauli hiyo, muda tu baada ya waziri wake wa shughuli za Baraza la Mawaziri, Luka Biong Deng, kujiuzulu wadhifa wake huo katika serikali ya Sudan hapo jana, akilalalamikia kile alichokitaja kuwa ni uhalifu wa kivita katika jimbo la Abyei, linalodhibitiwa na vikosi vya majeshi ya Kaskazini.
Deng, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, alisema walitaraji kuunda mataifa mawili yatakayokuwa na uhusiano mwema, lakini wenzao wa Kaskazini wanaonekana hawataki amani.
Mwanachama huyo wa chama cha Sudanese People's Liberation Movement (SPLM ), na ambaye anatokea jimbo hilo la Abyei linalokabiliwa na mzozo, amesema hawezi kuendelea kuhudumu katika serikali kuu ya Sudan kwa sababu vikosi vyake ndivyo vinavyofanya uhalifu huo wa kivita jimboni mwake.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema kiasi ya watu 15,000 wamekimbia ghasia katika eneo hilo la Abyei na hali inazidi kuwa tete.
Mwanzoni serikali ya Kaskazini mjini Khartoum ilikuwa imesema kuwa wanajeshi wake wako katika eneo hilo kurejesha utulivu tu, baada ya mashambulizi mabaya yaliyofanywa na vikosi vya Kusini Alhamis iliyopita.