1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama la umoja wa mataifa laidhinisha vikosi chad na afrika ya kati

26 Septemba 2007

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepitisha kwa kauli moja mpango wa kulinda maisha ya binadamu katika nchi zenye migogoro ya kisiasa ikiwemo Chad na eneo lote la Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/CB0x

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limetoa mamlaka ya kupelekwa majeshi ya Jumuiya ya Ulaya na polisi wa Umoja wa Mataifa zikiwa ni harakati za kulinda usalama wa raia katika nchi za Chad, Afrika ya Kati na Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Mamlaka hayo yametolewa chini ya kifungu cha sheria namba saba cha katiba ya Umoja wa Mataifa kinachotoa mamlaka ya kutumia nguvu za kijeshi kulinda maisha ya raia. Majeshi hayo yatakuwa katika maeneo hayo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Vikosi hivyo vya Umoja wa Ulaya na polisi wa Umoja wa Mataifa vitasaidia kuimarisha hali ya usalama kwa raia, kutoa misaada ya kibinadamu, kusaidia wakimbizi pamoja na waathirika wengine wa vita hiyo.

Mpango huo uliopitishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa pia utahusisha maofisa wa mashuala ya haki za binadamu, wawakilishi wa kijeshi, wawakilishi wa kijamii pamoja na wataalamu wa sheria.

Majeshi ya umoja wa ulaya na maofisa wa kipolisi wa umoja wa mataifa watasaidia kutoa mafunzo kwa polisi wa nchi hizo ili kudhibiti ulinzi katika makambi ya wakambizi.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Rais George Bush wa Marekani amesema hilo ndiyo suluhisho pekee na mpango waliofikia.

Rais Bush ameongeza kwamba hiyo ni hatua muhimu katika uelekeo uliokusudiwa na kwamba ndiyo njia pekee ya kutatua matukio ya mauaji nchini Chad, Afrika ya Kati na Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki Moon, amesema lengo la kutimiza mpango wa kurejesha usalama katika nchi zenye migogoro barani Afrika pia linahusisha Umoja wa Afrika.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Bwana Alpha Oumar Konare amesema anatumaini kwamba mpango huo utakwenda kama ulivyopangwa na vitendo zaidi kufanyika.

Bwana Konare amesema, ‘Masuala ya bara la Afrika yanaamuliwa kwa sehemu kubwa na Umoja wa Afrika. Tunataraji tutafikia haraka daraja na kuona mameno yakifuatiwa na vitendo. Ahadi chungu nzima zimetolewa hadi sasa kwa bara la Afrika’. Mwisho wa kumnukuu.

Mkutano huo pia umependekeza kuondoa kabisa vitisho na mauaji kwa wananchi wa Jimbo la Darfur nchini Sudan, baada ya kipindi kirefu cha mauaji na vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.

Licha ya mauaji makubwa yanayofanywa na wanamgambo wa Janjaweed Magharibi mwa Sudan, pia vitendo vibaya dhidi ya binadamu ikiwemo ubakaji, matumizi ya watoto katika uwanja wa vita na uporaji wa mali za wananchi vimekuwa vikitokea kwa wingi mno miongoni mwa raia wa Darfur.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki Moon, amesema vikosi vyenye jumla ya askari elfu 26 wakiwemo maofisa wa polisi wa kimataifa wanatarajia kwenda katika maeneo yenye migogoro. Jeshi hilo litakuwa kubwa la kwanza kutokea katika shughuli za kulinda amani duniani.

Naye Rais wa Ufaransa Bwana Nicolas Sarkozy, amesema bara la Afrika linazidi kuteketezwa na vita za wenyewe kwa wenyewe hali inayosababisha umaskini kupaa kwa kiwango cha kutisha.

Rais Sarkozy ameseema, ‘ Hatutastahiki kuachia umaskini uzidi kuenea barani Afrika, kwamba bara hilo lizidi kuteketezwa kwa vita na wakazi wake kuzidi kudhoofishwa na maradhi. Tukiacha, basi utulivu wa ulimwengu mzima utavurugika’. Mwisho wa kumnukuu.

Kama ilivyokuwa kwa Uingereza na Ujerumani, Ufaransa nayo ilihusika kwa kiasi kikubwa kuwa na makoloni mengi barani Afrika.

Aidha, Waziri wa nchi katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Bwana Kim Howell, ameitaka Sudan kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia uhalifu.