1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barabara za mji mkuu wa Togo zapewa majina mapya

P.Martin15 Februari 2007

Miaka miwili kufuatia kifo cha Gnassingbe Eyadema,rais aliengángania madaraka kwa takriban miongo minne,mambo sasa yanaanza kubadilika nchini Togo,barabara nyingi zikipewa majina mapya kuheshimu viongozi wengine wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CHK2

Taifa la Togo katika Afrika ya Magharibi sasa linaongozwa na Faure Gnassingbe ambae ni mtoto wa kiume wa marehemu Eyadema.Hilo halimaanishi kuwa mtindo wa kumtukuza baba yake umeendelea bila ya upingamizi.

Ukweli ni kuwa Faure Gnassingbe amezindua kampeni ya kufanyia ukarabati taswira za marais wengine wa zamani ambao baba yake alijitahidi kuwasahau, wakati wote aliokuwa akitawala.

Kwa mfano katika mageuzi yaliofanywa hivi karibuni,serikali imebadilisha majina ya barabara mbili za pwani katika mji mkuu Lome.Barabara hizo sasa zinaitwa “Sylvanus Olympio” kwa heshima ya rais wa kwanza wa Togo,alieuawa Januari 13 mwaka 1963.Gnassingbe Eyadema pia alihusika na mapinduzi hayo kwa sehemu kubwa.Lakini hakuingia madarakani mpaka yalipofanywa mapinduzi mengine, miaka minne baadae.Gnassingbe Eyadema,akashinda chaguzi za mwaka 1972,1979 na 1986 ambazo hazikuwa na wagombea wengine.Mkutano wa taifa mwaka 1991,ulijaribu kumshinikiza kuondoka madarakani lakini Eyadema aliomba msaada wa jeshi na kuanzia hapo,ndio alingángánia madaraka,hadi kufariki mwaka 2005 na hivyo kuwa kiongozi aliebakia madarakani muda mrefu kabisa barani Afrika.

Wakati wa utawala wake,mtu alipopita katika mitaa ya mji mkuu,ilikuwa sawa na kusoma historia ya kiongozi huyo.Kwa mfano,mtu alitoka uwanja wa ndege wa “General Gnassingbe Eyadema”,alipitia “Eyadema Boulevard” na alikwenda kutazama mpira katika uwanja wa michezo wa “Eyadema”.Njia nyingine iliitwa “Barabara ya Januari 13” kuadhimisha tarehe aliyoshika madaraka hapo mwaka 1967.”Barabara ya Januari 24” imeadhimisha tarehe ambayo ndege yake ya binafsi ilipata ajali.Mtindo huo wa kupigia debe heba yake,haukuishia kwenye majina ya barabara au hoteli kubwa za anasa.Kwani kulikuwepo pia saa za mkono zilizopambwa picha yake na kuuzwa Dola 20.

Sasa,miaka miwili baada ya kifo cha baba yake, Faure Gnassingbe alieshika madaraka katika uchaguzi wa mwaka 2005 uliozusha mabishano, ameamua kuwakumbuka marais wengine wa nchi hiyo kwa kuanza na Olympio.Hadi hivi sasa,mitaa na viwanja vinane vimepewa majina ya marais wa zamani kuambatana na ushauri wa halmashauri ya kitaifa iliyoundwa na Faure kama wananchi wa Togo wanavyopenda kumuita rais wao mpya.Sasa kiwanja kimoja maarufu kunapofanywa mikutano ya kisiasa na hata tamasha za muziki,kimepewa jina la waziri mmojawapo wa zamani “Anani Santos”.

Marais wa zamani hawatokumbukwa kwa heshima kwa kuipa mitaa majina yao tu bali kutakuwepo pia sanamu ya kila mmoja wao katika mji mkuu Lome.Hata shule,hospitali na majengo mengine ya umma yatapewa majina ya viongozi hao wa zamani.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa chama cha upinzani PDR,hatua hizo ni muhimu:ni vitendo vya kuona mbali kwa azma ya kuwapatanisha wananchi wa Togo.