1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi zaanza kuwaondoa raia wao Sudan Kusini

11 Julai 2016

Milio ya risasi ya hapa na pale imesikika leo mjini Juba, siku chache baada ya makabiliano mapya katika mji huo mkuu wa Sudan Kusini kusababisha maelfu ya wakaazi kukimbilia usalama wao

https://p.dw.com/p/1JMqg
Südsudan Opposition Soldaten
Picha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Milio ya risasi za bunduki za rashasha imesikika katika maeneo mawili ya Juba leo asubuhi, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa AFP na mfanyakazi mmoja wa mashirika ya msaada. Hapo jana mapigano makali baina ya jeshi na waasi wa zamani, yaliyohusisha vifaru, helikopta za kivita, makombora na maguruneti yakufyatuliwa na maroketi yalisababisha maelfu ya raia kuukimbia mji huo wakihofia usalama wao.

Makabiliano hayo, ya kwanza baina ya jeshi na waasi wa zamani mjini Juba tangu kiongozi wa waasi Riek Machar aliporudi nyumbani kuchukua wadhifa wa makamu wa rais katika serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Aprili, yalianza Ijumaa iliyopita wakati wanajeshi 150 walipouawa katika majibizano ya risasi. Vyombo vya habari nchini humo vinasema ni wanajeshi 270. Haijabainika wazi ni wangapi waliuawa katika machafuko ya jana Jumapili, ambayo yalikuja siku moja baada ya Sudan Kusini kuadhimisha mwaka wa tano wa uhuru.

Südsudan Präsident Salva Kiir und Vizepräsident Riek Machar
Riek Machar na Salva Kiir wanaombwa kuhimiza amaniPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Baraza la Makanisa la Sudan Kusini likiwawakilisha maaskofu wa nchini humo limetoa wito wa kuwapo utulivu kupitia redio.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezishinikiza nchi jirani za Sudan Kusini kusaidia kumaliza mapigano hayo, kwa kuitisha walinda amani zaidi na pia kuwataka Machar na Rais Salva Kiir kuwatuliza wanajeshi wao. Balozi wa Japan katika Umoja wa Mataifa Koro Besho ni rais wa Baraza hilo "Wanachama wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na ofisi za Umoja wa Mataifa na wafanyakazi ni uhalifu wa kivita. Pia wametoa wito kwa nchi za kanda hiyo, Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika na Jumuiya ya IGAD kuendelea kuzungumza na viongozi wa Sudan Kusini kutatua mgogoro huu".

Marekani imesema inawaondoa wafanyakazi wake wasiohusika na misaada ya dharura kutoka nchini humo na kuzitaka pande zote mbili “kuweka chini silaha” kurudi makambini na kuzuia machafuko zaidi na umwagaji damu.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini Michael Makuei aliwalaumu waasi wa zamani kwa kuzusha machafuko hayo, na akasisitiza jana kuwa serikali “ina udhibiti kamili wa mji mkuu Juba”. "Ni bahati mbaya kuwa tumepoteza maisha katika wakati ambapo hatukutarajia kupoteza watu wengi lakini hilo limetokea. Hata hivyo, tunasema acha twende kwa mpango wa amani, turejelee makubaliano hayo, ili tuanze kuyatekeleza.

Südsudan Flüchtlingslager Yida
Raia wanatoroka makaazi yao kutokana na vitaPicha: DW/L. Wagenknecht

Viongozi wa kikanda wakiwemo wa Kenya na Sudan wametoa wito wa kusitishwa mapigano na wanatarajiwa kuandaa mkutano maalum wa kilele mjini Nairobi leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema “ameshtushwa na kukasirishwa” na kurejea kwa mapigano na akatoa wito kwa pande zote mbili kusitisha vita.

Wafanyakazi wa misaada wanasema kambi moja ya Umoja wa Mataifa inawahifadhi karibu watu 28,000 waliokimbia makwao kutokana na mapigano hayo. Shirika la ndege la Kenya Airways lilisitisha jana safari zake za Juba, kwa sababu ya kile ilichokiita “hali ya usalama isiyotabirika”.

Mwandishi: Bruce Amani/
Mhariri: Gakuba Daniel