1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari za mzozo wa kifedha wa Marekani

P.Martin5 Septemba 2007

Hadi mwishoni mwa mwezi Julai,ni wataalamu tu walioijua Benki ya IKB ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CB1V

Lakini baada ya benki hiyo kujiepusha dakika ya mwisho kwenda muflisi,ilidhihirika kuwa mzozo wa Marekani kuhusu benki za mikopo ya nyumba,umefika hadi Ujerumani na hakuna siku iliyopita,bila ya habari mpya kuchomoza kuwa hiyo si benki pekee iliyoathirika.

Benki za Ujerumani kwa kiwango fulani, zimenusurika na mzozo wa kifedha uliozuka katika soko la mikopo nchini Marekani.Hayo ni maoni ya mameneja wengi wa benki kubwa za Ujerumani.

Kwa mujibu wa Josef Ackermann,mwenyekiti wa benki mojawapo kubwa nchini Ujerumani „Deutsche Bank“ hatua za haraka zilizochukuliwa kwa pamoja na serikali na benki,mwanzoni mwa mzozo huo, ziliisaidia benki ya IKB kutofilisika.

Kwani benki mbili za Ujerumani yaani SachsenLB na IKB,zilihitaji kusaidiwa na serikali na benki zingine za Ujerumani baada ya uwekezaji wa benki hizo mbili kwenda kombo katika sekta ya mikopo ya nyumba,nchini Marekani.

Ackermann,kwa mara nyingine tena,alizikosoa baadhi ya benki za Ujerumani kwa kusema kuwa mtindo wa kubahatisha kupindukia kiasi,ni tabia inayotia wasiwasi.Akaongezea:

„Sasa mfumo mzima unapaswa kusafishwa yaani wale waliofanya makosa waadhibiwe.Na hiyo ni kwa sote.Kwa maoni yangu hivyo ni sawa. „

Wakati huo huo,Ackermann alikubali kuwa kundi la benki yake pia liliathirika na mzozo wa mikopo ya nyumba uliozuka Marekani,lakini uongozi wao imara kuhusu hatari za aina hiyo,umeweza kuidhibiti hali iliyozuka.

Ackerman aliekuwa akizungumza kwenye mkutano wa benki mjini Frankfurt,alisisitiza umuhimu uliopo kwa benki na taasisi za kifedha kuungana katika makundi machache lakini yaliyo imara.

Sekta ya benki nchini Ujerumani,imegawika katika matawi kama matatu yaani,benki za binafsi,za umma na benki za ushirika.

Kufuatia mtikiso uliosababishwa na mzozo wa Marekani katika masoko ya kifedha duniani,kuna wasiwasi kuwa kutazuka mzozo mkubwa zaidi.Lakini mkuu wa benki,Ackermann amesema,tangu siku chache zilizopita kumekuwepo ishara kuwa masoko yameanza kutulia.

Yadhihirika kuwa matamshi yake yalisaidia kupiga jeki imani ya wawekezaji,kwani thamani ya hisa za Deutsche Bank iliongezeka kwa asilimia 2.4 katika Soko la Hisa mjini Frankfurt kinyume na hisa zingine.