1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad mfupa mgumu kwa Jumuiya ya Kiarabu

17 Oktoba 2011

Serikali ya Syria imeukataa wito wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu ulioitaka kukutana na wapinzani wake, huku mashambulizi ya vikosi vya serikali dhidi ya waandamanaji yakiendelea kwenye mji wa mpakani wa Zabadani.

https://p.dw.com/p/12tFT
Rais Bashar Al-Assad wa Syria
Rais Bashar Al-Assad wa SyriaPicha: dapd

Serikali ya Syria imesema inao uwezo wa kushughulikia mambo yake yenyewe na kwamba haitaitikia wito wa kwenda kwenye makao makuu ya Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu huko Cairo kuzungumza na wapinzani.

Mjumbe wa kudumu wa Syria kwenye Jumuiya hiyo, Balozi Yussuf Ahmed, amenukuliwa na Shirika la Habari la Syria (SANA) akisema kwamba ana mashaka na tamko la Jumuiya ya Kiarabu kujumuisha mualiko wa mazungumzo kati ya serikali na wapinzani.

"Syria ni taifa huru lenye mamlaka kamili na linaloongozwa na utawala halali wenye uwezo wa kuendesha mambo yote ya nchi. Mazungumzo yoyote yale lazima yafanyike Syria, yakiwa na ushiriki wa makundi yote bila ya kujali itikadi zao na ikiwepo Jumuiya ya Kiarabu, kwa mujibu wa makubaliano na utaratibu ulioridhiwa." Amesema Balozi Ahmed.

Maandamano dhidi ya Rais Assad barani Ulaya
Maandamano dhidi ya Rais Assad barani UlayaPicha: picture alliance/dpa

Kwa mujibu wa tamko la Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Hamad Al-Thani, ndiye atakayeongoza kamati maalum ya mawaziri wa mataifa ya Kiarabu kufanya kazi na serikali ya Syria kumaliza vurugu na mapigano ndani ya siku 15 zijazo. Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni mawaziri wa nje wa Oman, Sudan, Algeria na Misri.

Lakini Syria inapinga maneno yaliyotumika kwenye tamko hilo na pia mtu aliyeteuliwa kuingoza kamati hiyo, Sheikh Al-Thani wa Qatar, ambaye nchi yake inaonekana kuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono waandamanaji katika mataifa ya Kiarabu.

Hapo jana (16.10.2011), vikosi vya Syria viliushambulia mji wa Zabadani, ulio katika mpaka wa nchi hiyo na Lebanon, ikiwa ni siku moja tu baada ya mapigano makali kati ya vikosi hivyo na vile vilivyoasi.

Zaidi ya jumuiya 100 za kiraia, zilikuwa zimetoa tamko la kuitaka Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu kuitenga serikali ya Syria na kushirikiana Umoja wa Mataifa kwenye uchunguzi wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binaadamu. Umoja wa Mataifa unasema hadi sasa watu 3,000 wameshauawa, 187 kati yao wakiwa ni watoto.

Maandamano dhidi ya Rais Ali Saleh wa Yemen jijini Sanaa.
Maandamano dhidi ya Rais Ali Saleh wa Yemen jijini Sanaa.Picha: DW

Kwengineko kwenye ulimwengu wa Kiarabu, kiasi ya watu 23 wameuawa nchini Yemen, katika mapigano ya mwishoni mwa wiki kati ya vikosi vinavyomtii Rais Ali Abdullah Saleh na vile vinavyowaunga mkono waandamanaji.

Usiku wa kuamkia leo, waandamanaji wanane waliuawa na wengine 27 kujeruhiwa, wakati vikosi hivyo vilipokabiliana na wapiganaji wa Sheikh Sadeq al-Ahmar, wanaompinga Rais Saleh. Wanne kati ya waliouawa, walipigwa risasi katika uwanja wa Taghyir, ambapo waandamanaji wamepiga kambi kwa miezi kadhaa sasa.

Kiasi ya maroketi 10 yalirushwa kwenye uwanja huo, mojawapo likitua karibu sana na kliniki inayohudumia wahanga, kwa mujibu wa daktari mmoja wa kliniki hiyo. Mapigano makali yametokea kwenye mtaa wa Al-Hassaba, kati ya kundi la Al-Ahmar, na lile la Sheikh Saghir bin Aziz, ambalo limeendelea kumuunga mkono Rais Saleh.

Kwa mujibu wa hospitali inayomilikiwa na raia wa Kijerumani mjini Sanaa, kaka wa Aziz aitwaye Saleh ni miongoni mwa waliouawa baada ya risasi kupenya kichwani mwake.

Rais Saleh ya Yemen, kama ilivyo kwa Rais Bashar Al Assad wa Syria, wameendelea kusalia madarakani, licha ya maandamano ya miezi kadhaa dhidi yao, na huku kila dalili ikionekana kuwa Yemen na Syria zinaelekea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Saumu Yusuf