1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China zapinga azimio dhidi ya Syria

5 Oktoba 2011

Urusi na China zimepinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilioandaliwa na mataifa ya Ulaya na ambalo linatishia kuchukuwa hatua dhidi ya ukandamizaji wa serikali ya Syria kwa waandamanaji.

https://p.dw.com/p/12lpc
Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad wa Syria.
Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad wa Syria.Picha: dapd

Huku kukiwepo visa vipya vya watu kuuawa nchini Syria na nchi kadhaa zikitishia kuidhinisha vikwazo binafsi, kura za turufu za nchi hizo mbili zimezusha hasira za mataifa ya Ulaya yaliyopendekeza azimio hilo. Marekani imesema Baraza hilo limeshindwa kushughulikia changamoto ya dharura.

"Hakuna shaka, azimio hili sio kuhusu uvamizi wa kijeshi na halihusiki na suala la Libya, hiyo ni sababu isiyo na msingi kwa wale wanaoona afadhali kuuzia utawala wa Syria silaha, kuliko kusimama pamoja na raia wa Syria". Amesema balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice.

Nchi tisa zilipiga kura kuliunga mkono azimio hilo ambalo linatishia kuchukuwa hatua iwapo Rais Bashar al-Assad ataendeleza ukandamizaji wake dhidi ya waandamanaji, ambao Umoja wa Mataifa umesema umeshasababisha vifo vya kiasi ya watu 2,700.

Urusi na China zilitumia kura zao za turufu kama wanachama wa kudumu wa Baraza hilo kupinga azimio hilo.

Kabla ya kuanza kikao cha baraza hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid Muallem, aliyashukuru mataifa yaliyosimama pamoja na Syria.

Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad wa Syria.
Maandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad wa Syria.Picha: dapd

Afrika ya Kusini, India na Lebanon zilisita kupiga kura hiyo, jambo linalodhihirisha mgawanyiko katika Baraza hilo lenye wanachama 15 tangu Jumuiya ya Kujihami ya NATO ilipotafsiri Azimio kama hilo dhidi ya Libya kwa mashambulizi nchini humo.

Wanachama wengi waliopinga azimio hilo walitetea uamuzi wao kwa kulizusha suala la mashambulizi ya angani ya Libya na hofu kuwa huenda hilo likazuka tena nchini Syria.

Urusi imependekeza azimio mbadala linaloshutumu vurugu za upinzani pamoja na za serikali na linalotoa wito kwa majadiliano ili kumaliza mzozo huo. Mataifa ya Ulaya, hata hivyo, yaliahidi kuwa azimio hilo halitopigiwa kura.

Serikali za magharibi na mashirika wa kutetea haki za binaadamu zimeelezea kuongezeka shutuma kutokana na Baraza hilo kushindwa kupitisha azimio lolote kwa Syria, nchi ambayo tangu kati kati ya mwezi wa Machi, imetikiswa na maandamano ya kupinga utawala, ambayo Rais Assad amejaribu kuyazima kwa kutumia nguvu kali.

Katika vurugu za hapo jana, waangalizi wa haki za binaadamu nchini humo, wamesema kiasi ya watu 11 walipigwa risasi na kuuawa na vikosi vya usalama, wakiwemo watu sita katika jimbo lililopo kati, Homs, na wawili kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Canada imetangaza vikwazo vipya dhidi ya biashara ya mafuta ya Syria na uekezaji katika sekta hiyo, na imetangaza pia marufuku ya kusafiri na kuzuia mali ya watu 27 wanaosemekana kuwa karibu na Rais Assad.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayip Erdogan, aliunga mkono pendekezo la azimio la Umoja waMmataifa, na amesema nchi yake itatangaza hivi karibuni vikwazo dhidi ya nchi hiyo iliyo jirani yake.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE/DPAE
Mhariri: Oummilkheir Hamidou