1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA:Suala la waasi wa PKK kaskazini mwa Iraq lazidi kuzua mjadala

23 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7DL

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ali Babacan amekutana na uongozi wa juu wa Iraq akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Iraq Hoshiyar Zebari na kuwa na mazungumzo kuhusu suala la Uturuki kutaka kuwashambulia waasi wa kikurdi wa PKK.

Babacan amesema Uturuki inataka kufuata hatua zote za kidiplomasia na kisiasa na serikali ya mjini Baghdad kabla ya kuchukua uamuzi wa kijeshi dhidi ya waasi hao.

Jumuiya ya kimataifa pia imeitolea mwito Uturuki kujizuia kuwashambulia waasi hao.Uingereza ikitoa msimamo wake juu ya suala hilo waziri wake wa mambo ya nje David Milliband alisema

‚*Tumejitolea kikamilifu kuhakikisha kwamba kuna makubaliano ya kweli ambayo yanaruhusu serikali ya Uturuki kuwaambia watu wake kwamba jumuiya ya kimataifa na muhimu serikali ya Iraq wanalichukulia kwa uzito mkubwa suala hili.*

Rais George W Bush wa Marekani ameahidi ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuishawishi serikali ya Iraq kuchukua hatua dhidi ya waasi hao wa kaskazini mwa Iraq.

Aidha Rais Bush kwa upande mwingine ameitaka Uturuki kujizuia kuwashambulia waasi hao ambao wanadai wamewateka wanajeshi zaidi wakituruki.

Wakati huohuo maafisa wa kijeshi wa Uturuki wamesema wanajeshi wake wanane wametoweka baada ya mapambano na waasi wa PKK mwishoni mwa wiki ilkiyopita.