1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angela Merkel ateuliwa na rais wa shirikisho kuwa kansela

Oumilkheir Hamidou
5 Machi 2018

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amependekeza mbele ya bunge la shirikisho, Bundestag, Angela Merkel achaguliwe tena kuwa kansela. Pendekezo lake hilo linaambatana na kifungu nambari 63 cha sheria msingi.

https://p.dw.com/p/2tj0r
Angela Merkel CDU
Picha: Reuters/H. Hanschke

.

Kifungu hicho cha sheria ndicho kinachofungua njia ya kuchaguliwa kiongozi wa serikali. Anaechaguliwa ni yule mwenye kudhibiti idadi kubwa ya wabunge na sio tu wabunge waliohudhuria zoezi la kupiga kura. Ndio maana vyama vinavyounda serikali ya muungano hujitahidi kufanya kila liwezekano ili kuhakikisha wabunge wao wote wanahudhuria kikao cha kumchagua kansela.

Katika mhula wake huu wa nne kansela Merkel hatoweza kutegemea sauti nyingi kama ilivyokuwa alipopigiwa kura mwaka 2013. Serikali ya wakati ule ya muungano wa vyama vikuu au GroKo kama inavyoitwa ilikuwa na jumla ya wabunge 504 kutoka jumla ya wabunge 631 kaatika bunge la shirikisho Bundestag. Serikali hii mpya lakini ina wabunge 399 tu kutoka jumla ya wabunge 709. Kwa hivyo Marchi 14 wabunge wasiopungua 355 watabidi wampigie kura Angela Merkel aweze kuchaguliwa kuwa kansela.

Baada ya rais wa shirikisho kumpendekeza, kansela mteule Merkel ametilia mkazo umuhimu wa kuharakishwa mambo ili serikali mpya ipate kuwajibika ipasavyo."Itakuwa muhimu kuharakisha kwasababu serikali itakapoundwa tu , kazi inabidi ianze na mie kama kansela mteule, natumai nitachaguliwa, nitafanya kila niwezalo na kwa nguvu zangu zote ili serikali hii iwajibike ipasavyo mbele ya wananchi nchini Ujerumani."

Kansela Merkel  pamoja na rais wa Marekani Donald Trump na rais wa Urusi Vladimir Putin
Kansela Merkel pamoja na rais wa Marekani Donald Trump na rais wa Urusi Vladimir Putin

Ujerumani kushirikiana zaidi na Ufaransa barani Ulaya

Kansela Merkel ameahidi kuipatia Ujerumani sauti ya nguvu barani Ulaya kuweza kukabiliana na changamoto zinazousumbua umoja huo."Tunashuhudia kila siku jinsi Umoja wa Ulaya unavyotakiwa uwajibike na sauti ya nguvu ya Ujerumani kwa ushirikiano na Ufaransa na mataifa mengine wanachama ni muhimu." amesema kansela Merkel kabla ya mkutano wa kamati kuu ya chama chake cha Christian Democratic Union-CDU.

Miongoni mwa changamoto  zinazoukabili umoja wa ulaya , kansela Merkel ametaja vurugu katika biashara ya kimataifa, zinazochochewa na rais Donald Trump wa Marekani, na mzozo wa Syria ambako licha ya kwamba Umoja wa ulaya hauhusiki lakini unasababisha mikururo ya wakimbizi kuingia Ulaya, kwa wingi ambao haujawahi kushuhudiwa tangu mwaka 1945.

Wakati huo huo utafiti wa maoni ya wananchi unaonyesha kura ya ndio ya SPD kwa serikali ya muungano wa vyama vikuu imewapatia faraja. Idadi ya wanaokiunga mkono chama hicho imeongezeka na kufikia asili mia 19 huku CDU/CSU wakipoteza nukta moja na kubakiwa na asili mia 34.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/

Mhariri:Yusuf Saumu