1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani itategemea hatima ya nyumba 88 za Wapalestina zinazotarajiwa kuvunjwa

Sekione Kitojo6 Julai 2010

Mapambano ya mara kwa mara pamoja na hali inayoendelea ya wasi wasi katika eneo linalogombaniwa la Jerumani ya mashariki, wakaazi wanahofia inaweza kuzusha ghasia kubwa za kijamii.

https://p.dw.com/p/OC50
Mbunge wa bunge la Palestina Mohammed Abu Teir akizungumza wakati wa mahojiano na shirika la habari la AP nyumbani kwake mjini Jerusalem ya mashariki. Teir ni mmoja wa wabunge watano waliofukuzwa kutoka eneo hilo.Picha: AP

Mapambano ya mara kwa mara pamoja na hali inayoendelea ya wasi wasi katika eneo linalogombaniwa la Jerusalem ya mashariki wakaazi wa eneo hilo wanahofia inaweza kuzusha ghasia kubwa za kijamii.

Mapambano yanafuatia hatua ya Israel ya kuharakisha mipango ya kuvunja nyumba kadha za Wapalestina. Hii inaweza kusababisha wapalestina maelfu kadha bila makaazi.

Zaidi ya hayo , Israel inaendelea kuwavua maelfu ya Wapalestina wanaoishi katika eneo la Jerusalem ya mashariki uraia wao. Wajumbe wanne wa bunge la Palestina, PLC kutoka Jerusalem wameamriwa kuondoka nchini humo.

Silwan limekuwa eneo kuu la msuguano huo, katika eneo hilo linalotokota la Jerusalem ya mashariki. Hii inafuatia idhinisho la halmashauri ya jiji la Jerusalem la kuvunjwa kwa nyumba 22 za Wapalestina, na zingine 66 zikiwa katika orodha ya kungojea, ili kutoa nafasi kwa bustani ya Wayahudi pamoja na ujenzi wa nyumba za Wayahudi, yote hayo yakiwa ni kinyume na sheria za kimataifa.

Halmashauri ya jiji la Jerusalem inadai kuwa nyumba za Wapalestina zilijengwa bila ya kibali. Lakini Wapalestina wanakabiliwa na mpambano ambao unaonekana kuwa karibu unawazidi nguvu wa kiutendaji ili kuweza kupata vibali, licha ya uhaba mkubwa wa nyumba.

Wakati huo huo maafisa wa Israel wanahimiza kwa wazi ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika eneo la Jerusalem ya mashariki licha ya kuwa hii ni kinyume na maazimio ya umoja wa mataifa.

Kamati ya mipango na ujenzi ya wilaya ya mjini Jerusalem hivi karibuni itachapisha mpango mpya kuhusiana na upanuzi wa makaazi ya wayahudi katika Jerusalem ya mashariki, mengi yao katika ardhi inayomilikiwa na watu binafsi kwa upande wa Wapalestina.

Wanaweza kuleta matrekta yao na kuikanyaga familia yangu, Fakhri Abu Diab, mhasibu na msemaji wa kamati ya bustani inayojaribu kupambana na uvunjaji huo ameeleza . Hatutatoka majumbani mwetu. Ni afadhali nife kuliko kuona watoto wangu wakiwa hawana pa kukaa. Siko tayari kuishi katika hema ambalo pia huvunjwa kila mara amesema Abu Diab.

Kuvunjwa kwa nyumba hizo kutawaacha kiasi cha Wapalestina 1,500 wakiwa hawana mahali pa kwenda. Asilimia 62 ya watu ambao hawatakuwa na makaazi watakuwa watoto, anaongeza Abu Diab, baba wa watoto watano, na mmoja wa wakaazi ambao nyumba yake imepangwa kuvunjwa.

Wakaazi wa eneo la Silwan Bustan wamejaribu kuoanisha mipango ya maafisa hao wa halmashauri ya mji wa Jerusalem. Wamewaajiri wasanifu majengo kwa gharama kubwa ili kuanzisha mpango mbadala ambao utajumuisha maeneo kijani katika eneo la Silwan, na pia kuokoa nyumba za wakaazi hao.

Mipango hiyo ilikaliwa bila kuangaliwa kwasababu haiingiliani na mipango wa halmashauri ya kulifanya eneo hilo lionekane la Wayahudi zaidi, anasema Abu Diab.

Halmashauri ya mji wa Jerusalem imekana kata kata kuhusiana na uvunjaji wa nyumba na kuwaondoa Wapalestina kutoka Salwan, lakini haijaonyesha kiwango sawa cha nia kama hiyo kuhusu walowezi walioamriwa na mahakama za Israel kuondoka katika eneo hilo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / IPS

Mhariri:Abdul-Rahman