1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yakabiliwa na madeni ya kimataifa

John Juma30 Machi 2016

Miongoni mwa mataifa yanayokumbwa na tishio zaidi la kuongezeka kwa viwango vyao vya ukopaji kimataifa ni pamoja na Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Afrika ya Kati, Chad, Ghana na Mauritania.

https://p.dw.com/p/1IM50
Nigeria Symbolbild Korruption
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Baadhi ya mataifa ya Afrika yanakabiliwa na malimbikizi ya madeni. Hayo ni kwa mujibu wa wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi duniani. Mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yaliyokopa kimataifa sasa yanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi huku thamani ya bidhaa ikiporomoka.

Wataalamu wa uchumi wameelezea wasiwasi wao kuwa jinamizi la malimbikizi ya madeni limerejea kuyazonga mataifa ya Afrika, miaka ishirini tangu kufanywa kampeni duniani kote kufutilia mbali madeni yaliyoyakumba mataifa mengi masikini. Julien Marcilly, mchumi mkuu wa mashirika ya Coface nchini Ufaransa yanayotoa bima kwa mataifa yanayokabiliwa na madeni makuu kote duniani kuyaepusha dhidi ya kushindwa kulipa, amesema, watu hawakutarajia hali ya sasa kujitokeza na inazua wasiwasi mkubwa.

Mpango wa shirika la fedha duniani IMF ulioanzishwa mwaka 1996 hadi sasa umeidhinisha dola bilioni sitini na nane kusaidia mataifa 36 yasiyojiweza kulipa madeni yao ya kimataifa, 30 kati ya mataifa hayo yanatoka Afrika. Kinachotia hofu ni kwamba mataifa hayo yanaendelea kukopa madeni kwa viwango vya juu.

Baada ya kupata afueni ya kulipiwa madeni yao na mpango wa shirika la fedha duniani, baadhi ya mataifa yalifurahia uhuru wa bajeti zao kunawirisha uchumi ambao tayari ulikumbwa na bei za juu za bidhaa. Mchumi kutoka Tanzania Dr. Len Kasoga anasema hali hii imechangiwa na Afrika kuagiza bidhaa nyingi zaidi kuliko inazouza katika masoko makuu ulimwenguni miongoni mwa changamoto zaidi.

Chinesische Kleinunternehmer in Afrika
Picha: REBECCA BLACKWELL/AP/dapd

Katika miaka michache iliyopita, mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yameshiriki uuzaji wa bondi kama njia ya kujipatia fedha kuendeleza bajeti zao, mengine yakishiriki kwa mara ya kwanza. Hata hivyo ripoti ya karibuni kutoka shirika la viwango la Standard and Poors inasema si njia bora zaidi ikizingatiwa baadhi ya nchi ziliuza bondi zake wakati viwango vya thamani ya bondi vimeshuka.

Thamani ya sarafu za Afrika yadorora

Ripoti hiyo imeonya kuwa hali imebadilika na mataifa husika yatahitajika kutumia fedha zaidi katika miaka mitatu ijayo kulipa madeni yao, na kwamba mataifa mengi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara yatakumbwa na uamuzi mgumu kati ya kupunguza matumizi yao kifedha na kulazimika kulipa madeni kwa riba za juu siku za baadaye. Wakati huu madeni mengi yalitolewa na mashirika ya kibinafsi wala si shirika la fedha la kimataifa IMF au benki ya dunia.

Shirika la Standard and Poors linasema kudorora kwa thamani ya sarafu za mataifa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara, kunakohusishwa na kupungua kwa bei za bidhaa, kumechangia kuongezeka kwa viwango vya madeni katika sarafu za kimataifa.

Symbolbild Afrika Markt Bunt
Picha: C. de Souza/AFP/Getty Images

Utafiti uliofanywa na idara ya fedha nchini Ufaransa umeonyesha mpango wa shirika la Kimataifa la Fedha kwa ushirkiano na benki kuu ya dunia ulipunguza madeni ya mataifa 30 ya Afrika kutoka asilimia 119 hadi 33 kila mwaka.

Miongoni mwa mataifa 30 yaliyopata msaada kuwawezesha kulipa madeni ya kimataifa, 13 yameongeza viwango vyao vya mikopo kwa asilimia kumi kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ukopaji kwa kiwango cha juu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliongoza orodha hiyo kwa silimia 25, ikifuatwa na Niger kwa asilimia 23 na Malawi kwa asilimia 19.

Miongoni mwa mataifa yanayokumbwa na tishio zaidi la kuongezeka kwa viwango vyao vya ukopaji kimataifa ni pamoja na Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Afrika ya Kati, Chad, Ghana; Mauritania, Sao Tome na Principe.

Idara ya fedha nchini Ufaransa imesema hakuna njia ya mkato kuhusu mzozo wa madeni unaokumba mataifa ya Afrika. Huku ikionya mataifa mengine huenda yakarejelea hali ya awali miaka 20 kabla ulimwengu kufutilia madeni ya mataifa yasiyojiweza.

Kwa mujibu wa Carlos Lopez ambaye ni katibu mkurugenzi katika tume ya kiuchumi ya Afrika ndani ya Umoja wa Mataifa, jumla ya madeni ya Afrika yamechukua asilimia 38 ya sehemu ya ukuaji. Ameongeza kuwa madeni yataongezeka katika mataifa ambayo nidhamu zao kudhibiti bajeti ni dhaifu

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga