Afrika yaangaliwa vyengine na Ulaya | Masuala ya Jamii | DW | 17.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Afrika yaangaliwa vyengine na Ulaya

Ufahamu wa Ulaya kuhusu Afrika unategemea zaidi kinachosemwa na vyombo vya habari vya Kimagharibi kuhusu bara hili masikini lakini lenye rasilimali na watu wengi. Lakini sasa ufahamu huu unaanza kubadilika

Watoto wa Afrika

Watoto wa Afrika

Ufahamu walionao watu wengi kuhusu Afrika unatokana na kile wanachokiona, kukisoma na au kukisikia kupitia vyombo vya habari, ambavyo navyo mara nyingi huzungumzia yale mabaya tu ya Bara la Afrika, maana kwa wanahabari, taarifa mbaya ndiyo habari. Vita, njaa, uvunjaji wa haki za binaadamu na tawala za kimabavu ndiyo habari za kawaida. Kutoka uharamia kwenye bahari ya Somalia hadi mapambano ya waasi kwenye Niger Delta, taarifa kuhusu Afrika hazivutii sana.

Lakini je, ni kweli kuwa Afrika ina mabaya tu? Katja Dörner ni mbunge wa chama cha Kijani katika Bunge la Shirikisho la Ujerumani na alikuwemo kwenye ujumbe wa Bunge hilo kwenye ziara ya siku kumi kwenye nchi tatu za Mashariki ya Afrika: Kenya, Burundi na Djibouti, na alichokigundua ni tafauti kabisa na Afrika aliyojidhani anaijua. Anasema kwamba mtazamo wake wa mwanzo, sasa umebadilika.

Uharamia kwenye bahari ya Somalia

Uharamia kwenye bahari ya Somalia

"Mwanzo nilikuwa na mtazamo tafauti kuhusiana na hizi nchi tulizotembelea. Tulikwenda Djibouti, Kenya na Burundi na nilizikuta nchi hizo ziko tafauti kabisa. Watu wana hamu ya kuwajulisha mambo yao na wao pia wanaonekana kujua mambo mengi kuhusu Ulaya." Anasema Katja.

Yumkini Katja naye alikuwa amejengeka mawazo kwamba Afrika ni bara jeusi, lenye giza la migogoro, umasikini na njaa tu. Kwamba watu wake hawawezi kufikiri nje ya mipaka ya pua zao, lakini alichokikuta ni kwamba watu wana ufahamu mkubwa wa mambo, si yale tu yanayowahusu wao kama Waafrika, bali pia yale yanayoliunganisha bara lao na ulimwengu mzima.

Kwa mfano, suala la uharamia katika bahari ya Somalia ni tatizo linalotokea ndani ya Bara la Afrika, lakini lina mizizi yake nje ya bara hilo. Hivyo ndivyo wanavyoamini watu waliokutana na Katja na ndivyo sasa anavyoamini Katja mwenyewe pia.

"Tuligundua kwamba mazingira yaliyopo Somalia ni magumu sana. Takribani hakuna tena samaki baharini wa kuvuliwa na wavuvi wa Kisomali. Kwa hivyo, uharamia ni tatizo changamano sana." Anasema Katja

Na huu hapa ndio uchangamano wa tatizo hili: Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka huu, karibuni vyombo 200 vya kigeni vinavua kiharamu katika bahari ya Somalia. Matokeo yake ni kuwa, wavuvi wa Kisomali ambao hawana teknolojia ya kufika bahari kuu, wanajikuta hawana uwezo wa kuwapata samaki, na hivyo maisha yao yanaharibika. Kuzuia hilo, huelekeza hasira zao kwenye meli yoyote inayopita karibu yao. Wanakuwa wahalifu. Hao ndio sehemu kubwa ya wafungwa aliokutana nao Katja katika jela ya Shimo la Tewa, nchini Kenya.

Kwamba Afrika ina matatizo ni ukweli wa upande mmoja, lakini kwamba Waafrika hawana uwezo wa kutatua matatizo waliyonayo, ni jambo linalotiwa chumvi sana. Ziara hii ya wabunge wa Ujerumani barani humo, anasema mbunge Katja, imewafumbua macho kwamba Afrika kuna vipaji, uwezo na dhamira ya maendeleo. Kile kinachohitajika, ni Waafrika kupewa fursa ya kufanya hivyo na mifumo mikongwe ya kilimwengu.

"Kilichonivutia ni kwamba katika nchi zote tatu ni kuwa watu wana uwezo wa kujiendeleza wenyewe na kwa kweli wanataka kufanya hivyo. Mazungumzo yote tuliyokuwa nayo na watu, yanaonesha kwamba watu wana uwezo mkubwa na mawazo mazuri ya kujenga mustakabali wao. Lakini kwa upande mwengine, lazima ujuwe kwamba kwa mifumo iliyopo ni migumu sana kwao." Anamalizia Katja.

Mwandishi: Mohammed Khelef

Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QB3u
 • Tarehe 17.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QB3u

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com