1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI.

Abdu Said Mtullya20 Novemba 2011

Rais Michael Sata wa Zambia ataka Wachina walipe zaidi,

https://p.dw.com/p/13Dn4
Rais Michael Sata,wa Zambia( katikati) akizungumza na waandishi wa habari.Picha: AP

Wiki hii pamoja na masuala mengine, magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mvutano baina ya makampuni ya China na Rais Sata wa Zambia, juu ya kesi inayowakabili watuhumiwa wa ugaidi nchini Uganda na pia juu ya madai yaliyotolewa kuhusu sera ya nje ya Ujerumani juu ya wahalifu na madikteta wa Afrika wanaoishi nchini Ujerumani.

Juu ya mvutano uliozuka nchini Zambia baina ya Rais mpya wa nchi hiyo Michael Sata,na wamiliki wa migodi ambao aghalabu ni Wachina, gazeti la die tageszeitung limeripoti kuwa Rais mpya wa Zambia Bwana Sata ameanaza kuzitekeleza ahadi alizozitoa katika kampeni zake za uchaguzi. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Rais Sata alishinda katika uchaguzi mkuu kutokana na kura za maskini wa Zambia.

Rais huyo aliahidi katika kampeni yake ya uchaguzi, kuwaongezea Wazambia vipato. Na sasa baada ya kuingia madarakani ameanza kuichukua hatua ya kwanza. Amepandisha kodi ya mapato yanayotokana na migodi. Kuanzia sasa wamiliki wa migogi nchini Zambia watatoa asilimia sita ya mapato yao kwa serikali. Hapo awali makampuni ya migodi yalikuwa yanatoa asilimia tatu ya mapato kwa serikali.

Zambia inakusudia kuongeza bajeti katika sekta za afya, elimu na kilimo. Lakini hatua hiyo ya kuongeza kodi maana yake ni kupungua kwa mapato ya makampuni ya migodi ya China nchini Zambia. Gazeti la die tageszeitung limearifu katika makala yake kwamba sera mpya ya serikali ya Zambia inawafiki na maslahi ya wananchi, na hasa wanaofanya kazi wa migodi inayomilikiwa na makampuni ya China.

Gazeti die tageszeitung limekumbusha juu ya mgomo uliofanywa na wafanyakazi wa kampuni ya China Sino Metals mnamo mwezi wa Oktoba ili kudai nyongeza za mishahara. Gazeti hilo limesema sasa unakuja mwanga katika migodi ya Zambia!

Gazeti la die tageszeitung wiki hii pia limeripoti juu ya kesi inayowakabili watuhumiwa wa Ugaidi nchini Uganda ambayo imeahirishwa. Gazeti hilo limeripoti kuwa kesi hiyo ilisikilizwa kwenye mahakama kuu ya Uganda mjini Kampala, huku kukiwa na ulinzi mkali. Watuhumiwa hao wanakabiliwa na madai ya kufanya mashambulio ya mabomu yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 70 waliokuwa wanatazama fainali ya kombe la dunia mwaka jana.

Watu wengine 70 walijeruhiwa vibaya kutokana na mashambulio hayo. Mabomu hayo yaliripuliwa kati kati ya washabiki wa kandakanda waliokuwa wanaitazama fainali hiyo kwenye televisheni ya jumuiya mjini Kampala. Wanaitikadi kali wa kiislamu wa Somalia, al -shabaab walisema kuwa waliyafanya mashambulio hayo, kwa sababu Uganda imepeleka majeshi ya kulinda amani nchini Somalia, kuutekeleza mpango wa Umoja wa Afrika.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limechapisha mapitio ya kitabu kilichoandikwa na Markus Frenzel juu ya sera ya serikali ya Ujerumani kuhusu wahalifu na madikteta wa Afrika wanaoishi nchini Ujerumani. Katika kitabu hicho mwandishi huyo aliewahi kutunukiwa tuzo ya kutetea haki za binadamu na shirika la Amnesty International,anadai kwamba sera ya nje ya Ujerumani, pamoja na ya idara ya sheria juu ya wahalifu na madikteta hao hazilingani na uzito wa uhalifu wao.

Gazeti la Franfkurter Allgemeine limemkariri mwandishi huyo Markus Frenzel akitoa mfano wa Dr.Ignace Murwanashyaka aliekuja Ujerumani kama mwanafunzi mwishoni mwa miaka ya 1980. Baadae alikuja kuwa kiongozi wa kundi la waasi wa kihutu -FDRL waliokimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Katika kitabu chake Frenzel anadai kwamba Murwanashyka alitoa amri ya kufanya mauaji halaiki katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Alitoa amri hiyo kutokea mji wa Mannheim. Lakini idara za sheria za Ujerumani zilizipuuza taarifa juu ya shughuli za mtu huyo.

Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine limeyakanusha madai hayo kwa kusema kuwa mwandishi huyo amechagua kuzungumzia juu ya mkasa mmoja tu ambao hauiwakilishi sera yote ya Ujerumani juu ya wahalifu au madikteta wa Afrika wanaoishi nchini Ujerumani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ Josephat Charo