1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Charo Josephat24 Aprili 2009

Zuma ajiandaa kuingia ikulu ya Afrika Kusini huku maharamia wa kisomali wakifikishwa mahakamani huko Kenya

https://p.dw.com/p/HdGP
Kiongozi wa chama cha ANC nchini Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: AP

Uchaguzi wa Afrika Kusini ndio mada iliyohanikiza katika magazeti ya Ujerumani juma hili. Gazeti la Neues Deutschland liliripoti kuwa chama cha African National Congress kilikuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi huo huku upinzani ukiachwa na kazi ya kujaribu kukizuia chama hicho kupata thuluthi mbili ya wingi wa viti bungeni.

Gazeti la Berliner Zeitung lilimueleza mgombea wa chama cha ANC Jacob Zuma kuwa bwana mkubwa wa Afrika Kusini, nchi ambayo mhariri ameileza kuwa taifa la Ulaya barani Afrika. Gazeti limesema historia ya Afrika Kusini imeleta faida kubwa kwa taifa hilo lakini haihusiani hata kidogo na ukoloni mamboleo.

Desmond Tutu
Desmond TutuPicha: AP

Gazeti la Financial Times Deutschland lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema, "Nafurahi kwamba mimi si Mungu". Hayo ni maneno yake mshindi wa zamani wa tuzo ya Nobel, askofu Desmond Tutu wakati alipohojiwa na mhariri wa gazeti hilo. Bwana Tutu alikikosoa chama cha ANC wakati wa kampeni za uchaguzi na kusema ataaibika ikiwa mgombea urais wa chama hicho, Jacob Zuma, atakuwa rais. Hata hivyo Tutu amenukuliwa na gazeti la Finacial Times Deutschland akisema hana mbavu za kuuzuia ushindi wa bwana Zuma.

Maharamia mahakamani

Gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti habari kuhusu kesi dhidi ya maharamia tisa wa kisomali waliojaribu kuiteka nyara meli ya Ujerumani, MV Courier, mnamo Machi 3 mwaka huu katika ghuba ya Aden. Maafisa waliokuwa kwenye meli nyengine ya Ujerumani "Rheinland Pfalz" walikabiliana na maharamia hao na kuwakamata. Gazeti limesema maharamia hao wamesababisha hofu kubwa mjini Berlin kiasi kwamba serikali ya Ujerumani iliamua kuikabidhi kesi dhidi yao kwa mahakama kuu ya Kenya katika mji wa bandari wa Mombasa.

Mhariri amesema kesi hiyo imeanza kusikilizwa siku ya Jumatano juma hili mjini Mombasa chini ya waangailizi wa kimataifa. Lakini hata hivyo kuna wasiwasi ikiwa washukiwa hao wa uharamia watatendewa haki kutokana na kutiliwa shaka mfumo wa sheria nchini Kenya.

Nalo gazeti la Tageszeitung kuhusu kesi hiyo limesema haitakuwa ya haki. Mhariri amesema mfumo wa sheria nchini Kenya unakabiliwa na kesi nyingi mno na umezongwa na visa vingi vya rushwa. Hata balozi wa Ujeruamni nchini Kenya, Walter Lindner, ametaka kesi dhidi ya maharamia hao wa kisomali ifanyike katika viwango vya kimataifa. Andrew Mwangura, wa shirika la safari za baharini la Afrika Mashariki aliye mjini Mombasa amenukuliwa na gazeti la Tageszeitung akisema hajawahi kuona kesi ikifanywa kwa haki nchini Kenya.

Mungiki yaua

Gazeti la Neue Zürcher Zeitung liliripoti habari kuhusu mauaji ya watu 29 yaliyotokea wakati wa mapambano makali kati ya raia na wanachama wa kundi haramu la Mungiki katika mji wa Karatina, kilomita 90 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Wanachama wa kundi hilo waliwashambulia wakaazi wa mji wa Karatina usiku wa Jumatatu kuamkia siku ya Jumanne wiki hii, kwa kukataa kulipa kodi kwa usalama ambao kundi la Mungiki linasema limejitwika jukumu la kuwalinda wakaazi wa eneo hilo. Maiti zilizokuwa zimekatwa vichwa kutumia mapanga zilionekana zikiwa zimezagaa barabarani na kwenye mashamba ya migomba na majani chai.

Gazeti la Neue Zürcher Zeitung pia limearifu kuwa idadi kubwa miongoni mwa watu waliouwawa ni wanachama wa Mungiki ambao walishambuliwa na wakaazi wakati walipowavamia. Kundi la Mungiki linajulikana kwa tabia yake ya kuwalazimisha watu kulipa aina fulani ya kodi na huvunja upinzani wa aina yoyote kutumia vitendo vya kikatili na umwagaji damu.

Silaha haramu Darfur

Gazeti la Tageszeitung lilikuwa na kichwa cha habari kilichouliza: Je rais wa Libya kanali Muamar Gaddafi anaingiza silaha kisiri katika jimbo linalokabiliwa na mzozo la Darfur? Kampuni moja nchini Ubelgiji inataka kupeleka silaha nchini Libya, lakini mpaka sasa bado haijapata kibali cha kufanya hivyo. Mhariri wa gazeti hilo amesema tangu ijulikane kwamba Libya inataka kununua silaha kutoka Ubelgiji, kumezuka mzozo wa kisiasa mjini Brussels.

Gazeti la Tageszeitung linalochapishwa mjini Brussels, limeripoti kwamba serikali ya mjini Tripoli imeagiza silaha za thamani ya kiasi cha yuro milioni 11.5 kutoka kwa kampuni ya kutengeza silaha ya Nationale de Herstal nchini Ubelgiji. Miongoni mwa silaha hizo ni silaha ndogo ndogo zinazotumiwa katika mapigano ya upinzani.

Muammar Gaddafi
Rais wa Libya Muammar GadhafiPicha: AP

Eneo la Wallonia linalojitawala lenyewe nchini Ubelgiji, bado halijatoa uamuzi kwa hofu kwamba silaha hizo zitakapofika nchini Libya, huenda zikasafirishwa katika eneo la mzozo la Darfur nchini Sudan. Habari hizi tayari zimewahi kutolewa na wataalam wa Umoja wa Mataifa. Kwa mantiki hii Uingereza mwaka jana ilikataa kutoa leseni ya kusafirisha silaha nchini Libya. Kutoka nchini Sudan kwenyewe kuna tetesi kwamba kiongozi wa Libya, Muamar Gaddafi, anaipa silaha mbari ya Mahamid, ambayo ni sehemu ya wanamgabo wa serikali wa janjaweed wanaoshutumiwa kwa uhalifu wa kivita.

Machafuko Kongo

Gazeti la Tageszeitung pia lilikuwa na habari kuhusu machafuko ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mamia ya maelfu ya watu waliwakimbia waasi wa Kihutu kutoka Rwanda katika mkoa wa Kivu Kaskazini, liliandika gazeti hilo. Mhariri amesema matumaini ya kupatikana amani mashariki mwa Kongo yamepata pigo kubwa.

Menschen fliehen aus dem Kongo Goma
Maelfu ya watu wakiwakimbia waasi wa kundi la FDLRPicha: AP

Waasi wa kundi la FDLR katika siku za hivi karibuni wameimarisha mashambulio yao katika mkoa wa Kiu Kaskzini. Waasi hao walikishambulia kijiji cha Luofu usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi wiki iliyopita. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la misaada la Caritas katika eneo hilo, waasi hao walizichoma nyumba 255 na kuwachoma watu sita wakiwemo watoto watano.

Mhariri anasema shambulio dhidi ya kijiji cha Luofu lilikuwa kilele cha mfululizo wa mashambulio katika miji ya Kanyabayonga na Kirumba, kilomita 150 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma.

Mwandishi: Financial Times/Berliner Zeitung/Frankfurter Allgemeine

Mhariri: Saumu Mwasimba