1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo7 Desemba 2007

Viongozi wa Afrika wamuunga mkono rais Robert Mugabe kabla mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika nchini Ureno. Rais Mugabe kusomewa waraka kuhusu utawala bora.

https://p.dw.com/p/CYty
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Viongozi wa Afrika wameonyesha umoja kabla ya kufanyika mkutano kati yao na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Lisbon nchini Ureno.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung lilisema baada ya miezi sita ya mazungumzo serikali ya Zimbabwe ya chama cha ZANU PF imekubaliana na chama cha upinzani Movement for Democratic Change, MDC, kuhusu maswala ya chaguzi za bunge na rais zitakazofanyika mwaka ujao.

Katika hotuba yake kwa taifa Jumanne iliyopita, rais Robert Mugabe alizungumzia enzi mpya nchini Zimbabwe na kuzisifu juhudi za rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, ambaye aliteuliwa na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, mwezi Machi mwaka huu katika mkutano uliofanyika mjini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Rais Mugabe alisema atafanya mazungumzo ya maana na vyama vyote vya kisiasa bila vikwazo vyovyote lakini hakutoa maelezo ya kina. Alisema pia kwamba atawaruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka mataifa ya kigeni waingie Zimbabwe.

Rais Mugabe alisema mkakati wa Uingereza kutaka kuitenga Zimbabwe umeshindwa na anataka kugombea wadhifa wa urais mwezi Machi mwaka ujao.

Ingawa waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alisema hatohudhuria mkutano wa Lisbon iwapo rais Mugabe atahudhuria, sasa atamtuma mjumbe wake, waziri wa zamani wa misaada ya maendeleo, Barones Amos.

Gazeti la Handelsblatt lilisema Umoja wa Ulaya unataka kumsomea rais Mugabe taratibu za utawala bora wakati wa mkutano wa mjini Lisbon Ureno.

Mhariri wa gazeti hilo alisema Umoja wa Ulaya unataka kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na bara la Afrika lakini hauko tayari kunyamaza kimya kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu barani humo.

Katika mkutano wa mjini Lisbon wikendi hii kutafanyika mazungumzo ya ana kwa ana kati ya rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Gazeti lilisema kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika makao makuu ya umoja huo mjini Brussels Ubelgiji, kiongozi wa sera za kigeni wa umoja huo, Javier Solana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel ni viongozi waliotajwa kulifanya jukumu la kumsomea rais Mugabe waraka wa Umoja wa Ulaya kuhusu utawala bora.

Mzozo kuhusu rais Mugabe kuhudhuria mkutano wa Lisbon umeyatatiza matayarisho ya mkutano huo.

Mada ya tatu inahusu hatua ya rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, kumsamehe mwalimu wa kike kutoka Uingereza, Gillian Gibbons, Jumatatu iliyopita.

Gazeti la Frankfuter Allgemeine Zeitung lilisema maa huyo aliyehukumiwa kifungo cha siku kumi na tano na mahakama moja ya mjini Khartoum kwa kuwaruhusu wanafunzi wake waliite sanamu la dubu kuwa mtume Mohammad, aliruhusiwa aondoke Sudan.

Serikali ya Uingereza ilimtetea mama huyo ikisema hajawahi kuitukana dini ya kiislamu wala kuichukia dini yoyote ile. Gazeti lilisema kuruhusiwa kwa Gillian Gibbon arejee nyumbani kulimfurahisha waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown.

Mada ya nne inahusu hali ya wasiwasi katika mpaka wa Ethiopia na Eritrea. Gazeti la Neue Zürcher Zeitung lilisema mpaka uliokuwa uwekwe na mahakama ya Umoja wa Mataifa mjini The Hague Uholanzi haukuwekwa kwa muda uliokuwa umepangwa. Muda uliowekewa mahakama hiyo kukamilisha kazi hiyo ulimalizika mwishoni mwa mwezi uliopita. Tume iliyoundwa kushughulikia tatizo la mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea ilisema itajiondoa iwapo hakutakuwa na ushirikiano wa kuweka mpaka baina ya nchi hizo mbili.

Mhariri wa gazeti hilo alisema Ethiopia sasa imeizuia alama iliyowekwa katika mpaka wake na Eritrea.

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti ziara ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, nchini Ethiopia. Mhariri alisema Ethiopia imekuwa mshirika wa Marekani tangu mashambulizi ya Septemba 11 mwaka wa 2001 mjini Washington.

Marekani inaamini magaidi wanapata hifadhi katika eneo la pembe ya Afrika na ni serikali ya waziri mkuu Meles Zenawi pekee inayoonekana kukabiliana nao. Zenawi ambaye anajaribu kuwakandamiza wapinzani wake wa kisiasa anasaidiwa na Marekani kuleta uthabiti wa eneo zima la pembe ya Afrika. Lakini kufikia sasa hilo halijatimia. Ndio maana Condoleezza Rice alikutana na Meles Zenawi na viongozi wengine wa kiafrika mjini Addis Ababa Jumatano iliyopita.

Condoleezza Rice alisema mzozo kuhusu mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea unamsumbua sana na kutoa mwito utafutiwe ufumbuzi wa kisiasa haraka. Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anamalizia kwa kusema ziara ya siku moja ya Condoleezza Rice mjini Addis Ababa haikutosha kutuliza vita nchini Somalia, Sudan na jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, ambavyo vimekuwa vikiongezeka katika majuma yaliyopita.