1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo9 Desemba 2005

Mada zilizopewa kipambao mbele juma hili: tetemeko la ardhi latokea kwenye ziwa Tanganyika. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye ashatakiwa kwa ubakaji na kuwa mwanachama wa kudni la Lords Resistance Army, LRA. Makamu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini bwana Jacob Zuma naye ashtakiwa kwa ubakaji. Na Ivory Coast yapata waziri mkuu mpya.

https://p.dw.com/p/CHXc

Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumatatu iliyopita, lililitikisa eneo la mpakani kati ya Tanzania na jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema kwa mujibu wa habari zilizotolewa na wafanyakazi wa umoja wa mataifa, wakaazi kadhaa wa eneo hilo waliuwawa wakiwemo watoto, huku majengo makubwa yakitikiswa.

Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 6.8 katika vipimo vya Richter, na lilienea kufikia umbali wa kilomita 1,000 na kusababisha majengo marefu kutikisika mjini Nairobi, Kenya. Hakuna uharibifi wowote uliosababishwa na tetemeko hilo mjini humo, limesema gazeti hilo.

Mada ya pili inahusu mashtaka yanayomkabili kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda, Forum For Democratic Change, FDC, bwana Kizza Besigye. Gazeti la Frankfurterr Rundschau lilisema inadaiwa kwamba Besigye, mwenye umri wa miaka 49 na daktari wa maswala wa ukimwi, alimbaka mwanamke mmoja. Pia anatuhumiwa kuwa mwanachama wa kundi la waasi la Lords Resistance Army, LRA, ambalo linaendeleza matendo maovu kazkazini mwa Uganda.

Mkewe Besigye, Winnie Byanyima, amenukuliwa na gazeti hilo akisema shtaka la ubakaji dhidi ya mumewe ni upuuzi mtupu na ni uamuzi wa busara wa mumewe kutosema lolote kuhusu madai hayo. Besyige aliyakanusha mashtaka hayo mbele ya mahakama huku waandamanji wakikusanyika nje ya jengo la mahakama hiyo. Kwa wakati huu mikutano kama hii imepigwa marufuku nchini Uganda, hakuna mabiramu yaliyo na picha za Besigye yanayoruhusiwa kubandikwa na hakuna mijadala ya swala hili inayoruhusiwa katika redio.

Mada ya tatu inahusu mashtaka ya ubakaji yanayomkabili makamu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, bwana Jacob Zuma. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema kiongozi huyo anashtakiwa kwa kumbaka mwanamke aliye rafiki wa jamii yake na ambaye ni mwanaharakati mashuhuri wa ukimwi Forrest Town nyumbani kwake mjini Johanesberg. Mwanamke huyo wa umri wa miaka 31 anaugua ukimwi. Bwana Zuma ameyakataa madai hayo akisema yeye mwenyewe anapinga hujuma dhidi ya wanawake.

Kwa miezi kadhaa bwana Zuma amezungumziwa sana na vyombo vya habari tangu rais Thabo Mbeki alipomfuta kazi kama makamu wa rais katika serikali yake mwezi Juni. Hapo awali bwana Zuma alishtakiwa kwa ufisadi katika mahakama ya serikali. Wadadisi wa kisiasa wanasema kesi hizi zinazomkabili bwana Zuma ndio mwisho wa maisha ya kisiasa ya kiongozi huyo.

Kuhusu mada hii gazeti la Die Welt lilisema watu hawakuruhisiwa mahakamani wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya bwana Zuma, ambaye bila shaka angechukua uongozi wa Afrika Kusini baada ya rais Mbeki. Polisi walitumwa kushika doria nje ya mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea.

Mada ya nne ilihusu kuteuliwa kwa waziri mkuu mpya nchini Ivory Coast. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema rais Laurent Gbagbo hakuwa na la kusema wakati rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria alipomtangaza aliyekuwa gavana wa benki kuu nchini Ivory Coast, Charles Konan Banny kuwa waziri mkuu mpya. Umoja wa mataifa na umoja wa Afrika unataka hatimaye kiongozi huyo achukue baadhi ya madaraka na kuyapunguza mamlaka ya rais.

Rais Gbagbo pamoja na waasi wa kazkazini mwa nchi hiyo walijaribu kuzuia uteuzi wa waziri mkuu huyo wa serikali ya mpito. Haijulikani lakini ikiwa rais Gbagbo atamkubali kiongozi huyo ambaye anakabiliwa na jukumu kubwa la kuliondoa taifa kutokana na vita vya wenyewe wa kwa wenyewe na kuandaa uchaguzi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Uchaguzi mkuu nchini Ivory Coast unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka ujao na waziri mkuu haruhusiwi kugombea wadhifa wake. Waasi wa kazkazini wanaunga mkono kuahirishwa kwa uchaguzi uliokuwa ufanyike hapo awali, lakini wanapinga kuruhusiwa kwa Gbagbo kuendelea kutawala. Waasi wanatambua uteuzi wa Konan Banny kama waziri mkuu mpya.