Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 27.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Siku ya Malaria Afrika iliadhimishwa Jumatano iliyopita. Gazeti la Berliner liliripoti kwamba katika nchi za joto watu kati ya milioni moja na milioni mbili hufariki dunia kutokana na malaria, asilimia 90 kati yao wakitokea barani Afrika. Aina hatari kabisa ya ugonjwa huu huitwa ´malaria tropica´ na ina uwezo wa kumuua mtoto mchanga katika muda wa saa chache.

Kwa mujibu wa shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, mtoto mmoja hufariki dunia barani Afrika katika kila sekunde 30. Ugonjwa huu unapotibiwa mapema mgonjwa aweza kupona.

Viongozi wa serikali barani Afrika walikutana mjini Abuja Nigeria mnamo tarehe 25 mwezi Aprili mwaka wa 2000 na wakakubaliana kushirikiana kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa malaria. Ndio maana siku ya malaria barani Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 mwezi Aprili.

Mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda duniani G8 bara la Afrika linahitaji fedha na wala sio malengo mapya ya maendeleo. Hayo yaliripotiwa na gazeti la Tageszeitung. Mhariri wa gazeti hilo alisema mataifa ya G8 yalikubaliana katika mkutano wao uliofanyika mjini Gleneagles kutoa dola bilioni 50 kwa Afrika kufikia mwaka wa 2010. Lakini miaka miwili baada ya mkutano huo, na huku mkutano mwingine wa kilele ukikaribia, hakuna mengi yaliyofanyika. Ni asilimia 10 pekee ya fedha walizoahidi ambazo zimekusanywa.

Gazeti la Tageszeitung liliendelea kusema jukumu sasa linamlalia kasela wa Ujerumani Bi Angela Merkel, ambaye Jumatano jioni alikutana na waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, mjini Berlin hapa Ujerumani.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kutafuta njia za kutimiza ahadi za mkutano wa Gleneagles kwenye mkutano wa kilele utakaofanyika mjini Heiligendamm. Hata hivyo kansela Angela Merkel alinukuliwa na gazeti hilo akitaja vikwazo vipya na kusema ipo haja ya kufanya jitihada za kuyafikia malengo yaliyowekwa kulisaida bara la Afrika.

Umoja wa Ulaya una wasiwasi mkubwa kuhusu hali katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Gazeti la Frankfurter Allgemenine lilisema kufuatia taarifa iliyotolewa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Jan Elliansson, mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya walielezea wasiwasi wao juu ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jimbo la Darfur, wakati walipokutana mjini Luxembourg Jumatatu iliyopita.

Mhariri alisema kwa kuwa serikali ya Sudan ilikubali wanajeshi 3,000 wa Umoja wa Mataifa wapelekwe Darfur kukisaidia kikosi cha Umoja wa Afrika kinacholinda amani Darfur, Umoja wa Ulaya uliamua kuchelewesha vikwazo ulivyotaka kuiwekea Sudan. Hata hivyo Umoja huo umetaka vikwazo dhidi ya Sudan vijadiliwe kwanza na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Gazeti la Frankfurter Rundschau lilikuwa na habari juu ya kuuwawa kwa mamia ya Wasomali kwenye mapigano mjini Mogadishu. Msemaji wa shirika lisilo la kiserikali mjini humo, Civil Society in Action, bwana Abdulahi Shirwa, aliliambia gazeti hilo kwamba majeshi ya Ethiopia yameuharibu kabisa mji wa Mogadishu akisema hakuna mji ulioharibiwa kiasi hicho tangu kumalizika vita vya pili vya dunia.

Abdulahi Shirwa alitoa mwito waangalizi watumwe Somalia kufanya uchunguzi ili kulifungulia mashtaka jeshi la Ethiopia kwenye makahama ya mjini The Hague, Uholanzi. Mashirika ya kutoa misaada yameitolea mwito mahakama ya uhalifu wa kivita mjini The Hague iwafungulie mashtaka wanajeshi wa Ethiopia kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Gazeti la Neue Zürcher linatukamilishia na habari za shambulio la waasi katika eneo la Ogaden nchini Ethiopia. Waasi wa kundi la Ogaden National Liberation Front, ONFL, waliwaua watu 74 mashariki mwa Ethiopia na kuwateka nyara wafanyakazi saba wa mafuta kutoka China. Miongoni mwa waliouwawa walikuwa Waethiopia 65 na Wachina 9 waliokuwa wakitafuta mafuta katika eneo la Ogaden. Shambulio hilo la waasi lililenga kuvuruga kazi ya kutafuta mafuta katika eneo hilo.

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusu kisa hiki liliripoti kwamba Ethiopia iliishutumu Eritrea kwa shambulio hilo la waasi wa Ogaden.
 • Tarehe 27.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHT6
 • Tarehe 27.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHT6