1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD yaongoza dhidi ya CDU katika jimbo la Saxony

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2024

Utafiti wa kura za maoni unaonyesha kuwa chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD kinaongoza dhidi ya chama cha Christian Democratic Union CDU katika jimbo la Saxony, ikiwa ni miezi 9 kabla ya uchaguzi wa jimbo hilo.

https://p.dw.com/p/4anU4
Chama cha AfD
Chama mbadala kwa Ujerumani cha AfDPicha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Utafiti wa kura za maoni uliotolewa Jumanne unaonyesha kuwa chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD kinaongoza dhidi ya chama cha Christian Democratic Union CDU katika jimbo la Saxony, ikiwa ni miezi 9 kabla ya uchaguzi wa jimbo hilo.

Soma pia: Chama cha Ujerumani AfD kujiimarisha siasa za Ulaya

Katika utafiti wa kura za maoni za mtandaoni uliofanywa na taasisi ya utafiti wa maoni ya Civey na Gazeti la Saxony, Sächsische Zeitung, AfD ilipata asilimia 37 ikilinganishwa na asilimia 33 za CDU.

Mwezi mmoja uliopita, vyama hivyo viwili vilikuwa vimekabana koo katika jimbo hilo kwa mujibu wa utafiti huo.

Alice Weidel
Kiongozi mwenza wa AfD Alice WeidelPicha: Leonhard Simon/Getty Images

Chama cha Social Democratic SPD cha Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani sasa kiko katika asilimia 3 na kiko hatarini kutoingia katika bunge la  jimbo hilo, kwa kuwa kunahitajika asilimia 5 kama kiwango cha chini.

Chama kinachounga mkono biashara cha Free Democratic Party FDP, ambacho pia kiko katika muungano wa serikali ya shirikisho, sasa kina asilimia 1.

Chama cha kijani ambacho pia kiko katika muungano tawala kina asilimia 7 huku chama cha mrengo wa kushoto kinapewa asilimia 8 na pia kiko nyuma ya AfD na CDU katika jimbo hilo ambalo linajumuisha miji mikubwa ya Leipzig na Dresden.

Wapiga kura katika jimbo la Saxony watapiga kura Septemba mosi mwaka huu.