1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Waasi kuwaachia mateka wa Kichina

27 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6m

Waasi wa Ethiopia ambao waliwauwa watu 74 na kuwateka nyara wafanyakazi saba wa Kichina katika shambulio kwenye machimbo ya mafuta wamesema hapo jana hawana mipango ya kuwashikilia mateka hao au kushambulia makampuni mengine ya kigeni.

Msemaji wa kundi la Ukombozi wa Taifa la Ogaden alieko London Uingereza amesema kundi hilo limewaonya wawekezaji kwamba eneo hilo ni la vita na kwamba wanataraji mzozo huo kupamba moto.

Abdirahim Mohammed Mahdi amesema kwamba licha ya kuwa hawana mipango mipya kwa sasa kushambulia kampuni za kigeni sera yao ya jumla ni kwamba wageni hawaruhusiwi kuchimba mafuta au gesi huko Ogaden na kampuni yoyote itakayofanya hivyo itawajibika kwa kitakachotokea.

Waasi hao wanaotaka kujitenga ambao wamekuwa wakipambana na serikali ya Ethiopia tokea mwaka 1984 walivamia machimbo ya mafuta yalioko chini ya usimamizi wa China kusini mashariki ya Ethiopia hapo Jumanne na kuuwa Waethiopia 65 na Wachina tisa.