1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zidane: nitaweka moyo na nafsi katika Real

5 Januari 2016

Nguli wa Real Madrid Zinedine Zidane ameahidi kuuweka “moyo wake na nafsi yake” katika kuwaongoza miamba hao wa Uhispania baada ya kuteuliwa katika hatua ya kushangaza kuwa kocha mpya kufuatia kutimuliwa kwa Rafa Benitez

https://p.dw.com/p/1HY23
Spanien Zinedine Zidane und Florentino Perezin Madrid
Picha: picture-alliance/dpa/V. Lerena

Mshindi huyo mara tatu wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka anachukua usukani katika klabu hiyo tajiri zaidi ulimwenguni licha ya kuwa na ujuzi mdogo wa ukufunzi ambao ulitokana na kuiongoza klabu ya daraja ya pili ya Real Madrid, Castilla. Lakini Zidane mwenye umri wa miaka 43, amesema atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa Real, ambayo sasa inashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu ya kandanda ya Uhispania La Liga baada ya kuwa na kipindi kisichokuwa na furaha chini ya Benitez, inashinda taji msimu huu.

“tuna klabu bora duniani, mashabiki wazuri sana na tunachostahili kufanya sasa, na nitakachojaribu kufanya kadri nnavyoweza, ni kuhakikisha kuwa timu hii inashinda taji mwishoni mwa msimu”, amesema Mfaransa huyo.

Muda wa mkataba wa Zidane haukutangazwa. Sasa yeye ndiye kocha wa 11 kuteuliwa chini ya rais wa Madrid Florentino Perez, ambaye mihula yake miwili ya uongozi imemaliza miaka 12.

Perez amesema ulikuwa uamuzi mgumu kumfuta kazi Benitez, ambaye uongozi wake wa miezi saba ulimalizika baada ya sare ya 2-2 na klabu yake ya zamani Valencia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo