Ziara ya waziri wa nje wa Ujerumani Moscow | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya waziri wa nje wa Ujerumani Moscow

Mawaziri wa nje wa Ujerumani Bw.Steinmeier na wa Marekani dr.Rice walikuwa jana na mazungumzo na rais Putin mjini Moscow.

Bw.Steinmeier na rais Putin

Bw.Steinmeier na rais Putin

Mawaziri wa nje wa Ujerumani Bw.Steinmeier na waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleezza Rice katika mazungumzo yao hapo jana mjini Moscow na rais Putin, miongoni mwa watu wengine, walijaribu kupunguza mvutano ulioibuka wiki chache nyuma kati ya Russia upande mmoja na kambi ya nchi za magharibi kwa upande wapili.

Hata ingawa hakujakuwa na matokeo barabara,pande zote mbili zimesisitiza kwamba zina hamu ya kuwa na usuhuba mwema na mwenzake na ungependelea kuacha kutoa maneno makali.

Kwahivyo, alao hali ya hewa imepambazuka kutokana na mikutano hiyo 2 ya mawaziri wa nje mjini Moscow.Pande zotre mbili zimejitahidi kuondoa mawingu yaliotanda katika uhusiano wao.

Kwani, tangu mazungumzo aliofanya waziri wa nje wa Ujerumani Bw.Frank-Walter Steinmier hata yale ya waziri wa nje wa Marekani Dr.Rice juu ya mada zilizozusha mabishano makubwa wiki chache nyuma,kila upande umetaka mambo yasiachwe kuharibika zaidi.

Mwanzoni mwa mazungumzo kati ya Rais Wladmir Putin na Bw.Steinmeier,rais wa Russia alieleza kwamba, Ujerumani mwaka huu imejitwika mizigo 2 –mmoja ni jukumu lake kama mwenyekiti wa kundi la dola 8 za kiviwanda-G-8 na mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya.Russia, alisema rais Putin, itayari kuiungamkono Ujerumani katika jukumu hilo.Isitoshe, rais Putin alisema:

“Tumshukuru Mungu kwamba, hatuna ugomvi kati yetu.Ndio, tuna mawazo yanayo tofautiana kuhusu vipi kuyatatua matatizo yaliochomoza.Lakini, pande zote mbili zina hamu kuona matatizo haya yanatatuliwa.Kwa maoni yangu, tayari si hali mbaya.”

Waziri wa nje wa Ujerumani Bw.Steinmier, alifunga jana safari ya Moscow akiitikia mualiko wa waziri mwenzake wa mambo yanje wa Russia Lavrov.

Madhumuni ya mualiko huo, ni kuzungumza juu shida zilizochomoza katika uhusiano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya kabla ya mkutano ujao uliopangwa ijumaa hii mjini Samarra,Russia.Azma hasa ya mkutano huo wa kilele huko Samarra, ni kuanzisha ushirika mpya kati ya UU na Russia.Lakini, Poland, mwanachama mpya wa UU anatia munda kwavile, Russia imeiwekea Poland marufuku ya nyama yake kusafirisha Moscow tangu mwishoni mwa 2005.

Matokeo wazi ya mazungumzo yao hakuna .Iwapo mazungumzo ya jana yameweka masharti mema kwa mkutano wa kilele kati ya UU na Russia,ni kusubiri kuona.

Dr.condoleeza Rice ,alikutana pia hapo jana na

Rais Putin pamoja na waziri wake wa nje Lavrov.Rice alijaribu kuiondolea Russia wasi wasi juu ya mradi wake wa kuegesha makombora ya Marekani karibu na mpaka na Russia.

Ajenda nyengine ya mazungumzo yao, ni swali la uhuru wa Kosovo,ambao Russia haitaki kabisa kuridhia.

Marekani na Russia,zinataka sasa kupita njia za kibalozi kumtuliza shetani.Uhusiano kati ya Moscow na Washington uligubikwa karibuni na kelelel nyingi kutoka kila upande juu ya mradi huo wa makombora na mada nyengine za kutatanisha kati yao.

Dr.Condoleeza Rice alipowasili Moscow hapo juzi, alibainisha wazi kwamba, licha ya mvutano uliopo kati ya Russia na Marekani,huwezi kusema ni kufufuka kwa vita baridi.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com