1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya kwanza ya rais wa DRCongo Tshisekedi Ubeligiji

Oumilkheir Hamidou
17 Septemba 2019

Rais Felix Tshisekedi wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo yuko ziarani Ubeligiji kwa lengo la kurejesha uhusiano wa kawaida pamoja na wakoloni hao wa zamani , baada ya miaka kadhaa ya mivutano .

https://p.dw.com/p/3PiGf
DR Kongo Felix Tshisekedi beim Kinshasa Digital Forum
Picha: Präsidentschaft der DR Kongo/G. Kusema

Felix Tshisekedi ameshafika ziarani April iliyopita mjini Washington ambako  alikutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo.

Lakini  ziara yake hii nchini Ubeligiji ni ya kwanza barani Ulaya tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais decemba 30 mwaka  2018 katika jamahuri ya kidemokrasi ya Congo.

Awamu rasmi ya ziara hiyo iliyoanza jumatatu usiku, inaanza jumanne hii ambapo rais Tshisekedi na mkewe wamealikwa karamu ya chakula cha mchana pamoja na mfalme Philippe na mkewe malkia Mathilde kabla ya kuhutubia viongozi wa shirikisho la wanaviwanda wa Ubeligiji mjini Brussels.

Jumatano rais Tshisekedi atautembelea mji wa kaskazini wa Anvers ambako amepangiwa kukutana na wakuu wa viwanda vya almasi.

Alkhamisi amepangiwa pia kukutana na mwenyekiti anaemaliza mhula wake wa Halm ashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean Claude Juncker.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji Didier Reynders
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji Didier ReyndersPicha: Imago Images/Belga/B. Doppagne

Ubeligiji na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zadhamiria kurejesha uhusiano wa kawaida

Kwa maoni ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji, Diedier Reyndres aliyempokea rais Tshisekedi alipowasili jumatatu usiku katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Melsbroek, karibu na Brussels, ziara hii imelengwa kusawazisha "hatua baada ya hatua" uhusiano uliopooza tangu mwaka 2015 kutokana na kiu cha rais wa zamani Joseph Kabila cha kutaka kugombea mhula wa tatu hadi alipoamua hatimae  Agosti mwaka 2018 kutogombea tena wadhifa huo, uamuzi uliosifiwa wakati ule na Ubeligiji.

Lakini miezi kadhaa ilipita kabla ya watawala hao wa zamani wa Ukoloni kuyatambua matokeo yaliyobishwa ya uchaguzi ambapo chama cha Kabila kinadhibiti wingi wa viti bungeni na wafuasi wake wanashikilia nyadhifa muhimu serikalini."Tunatambua kwamba uhusiano kati ya nchi zetu umekumbwa na misuko suko, tutajaribu kuurekebisha hatua baada ya hatua na bila ya pupa" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubeligiji Didier Reynders katika mahojiano na gazeti la La Libre Beligique.

Kwa upande wake rais Tshisekedi amesema anataraji ziara hii itasaidia kuanzishwa upya ushirikiano wa kijeshi na ahadi za misaada ili kuimarisha mifumo ya afya na elimu nchini mwake.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri-Yusuf Saumu