Ziara ya kansela Merkel barani Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya kansela Merkel barani Afrika

Kansela Merkel anapanga kuzitembelea zile nchi zilizopiga hatua kubwa mbele katika kuleta mageuzi

default

“Mjadala bayana na wa kuambiana ukweli pamoja na waafrika” ndio anaoudhamiria kansela wa Ujerumani Angela Merkel ,katika ziara yake hii ya kwanza barani Afrika.Mwenyekiti huyo wa jumuia ya mataifa tajiri kiviwanda G8 anaanza hii leo ziara ya siku nane itakayomfikisha Ethiopia,Afrika kusini na Liberia.

Katika mahojiano pamoja na Bob Geldorf,pembezoni mwa mkutano wa kilele wa jumuia ya mataifa tajiri kiviwanda G8,kansela Angela Merkel alizungumzia maendeleo na matumaini mema yaliyochomoza katika nchi nyingi za Afrika.

Ndio maana ziara hii ya kwanza ya kansela wa Ujerumani katika bara jirani imelenga mataifa yaliyopiga hatua muhimu mbele katika kuleta mageuzi na kutoa mfano mzuri wa kuigizwa.

Afrika kusini,mshirika mkubwa wa kiuchumi wa Ujerumani,Ethiopia yanakokutikana makao makuu ya Umoja wa Afrika unaopania kuimarisha amani na demokrasia barani humo na Liberia iliyojikomboa toka janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kule tuu ambako viongozi wana moyo wa kisiasa na taasisi zinazohitajika ndiko misaada ya maendeleo inakoweza kuleta tija,anaamini kansela Angela Merkel:

“Bila shaka kwa mtazamo wa umma,vita dhidi ya umasikini ni muhimu kabisa.Na hilo ndilo lengo la ushirikiano wa maendeleo.Lakini tumegundua kwamba tunaposimamia tuu miradi ya kupambana na umasikini,bila ya kuwepo miundo mbinu na taasisi zinazohitajika kuweza kufikisha fedha kwa wananchi-basi tutakua tunatoa mafedha tuyatakayo ya kupambana na umasikini bila ya kulifikia lengo la kuung’owa umasikini.Ikiwa nchi zitazongwa na balaa la rushwa,na ikiwa fedha zitatolewa kugharimia miradi isiyokua na maana,hapo pia hakuna faida.Inamaanisha:pekee zile nchi ambazo zinahakikisha aina fulani ya usalama kwa raia zake,ambako pesa hazitapotelea mahala kusikojulikana,ambako wananchi waliokombolewa toka hali ya umaskini wanajivunia pia haki,huko tuu ndiko umaskini unaweza kukoma milele.”Amesema hayo kansela wa ujerumani bibi Angela Merkel

Liberia inayongozwa na rais mkakamavu bibi Ellen Johnson Sirleaf aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi na Afrika kusini ni mfano mzuri wa mataifa yaliyofanikiwa kutia njiani mageuzi barani Afrika,na ambako demokrasia na sheria zinaheshimiwa.

Mataifa hayo ndiyo yatakayofaidika zaidi na misaada ya maendeleo anasisitiza kansela Angela Merkel.

Utawala bora na mageuzi ya kisiasa ni miongoni mwa malengo ya Umoja wa Afrika.Kansela Angela Merkel anaanza ziara yake kwa kuyatembelea makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Abeba nchini Ethiopia.Mazungumzo yake hii leo pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba,yatagusia pia mzozo wa Somalia,Sudan na Tchad.

Ziara ya kansela Angela Merkel inafanyika pia kwa niaba ya jumuia ya mataifa tajiri kiviwanda G8.Kansela Angela Merkel ambae ndie anaeiongoza jumuia hiyo ameorodhesha masuala ya bara la Afrika mstari wa mbele kabisa wa ajenda ya jumuia hiyo.

Kansela Angela Merkel amedhamiria kutekeleza ahadi zilizotolewa na jumuia hiyo kivitendo.Kwa mwaka 2008 msaada wa maendeleo wa Ujerumani kwa Afrika unapngezeka na kufikia yuro milioni 750.

Ziara ya kansela Angela Merkel barani Afrika imelengwa kuzidisha hadhi ya Ujerumani barani Afrika ,baada ya kujiweka kando kwa miaka kadhaa panapohusika na siasa ya nje ya Ujerumani kuelekea bara hilo jirani.

Hadhi hiyo imeanza kuimarika kufuatia ziara za mara kwa mara za rais wa Shirikisho Horst Köhler na waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinemeier mwezi Agosti uliopita.

 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Ute Schaeffer/Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7I
 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Ute Schaeffer/Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7I

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com