1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky aahidi ushindi dhidi ya Urusi

Lilian Mtono
24 Februari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameapa kwamba Ukraine itaishinda Urusi kwenye vita baina yao vinavyoingia mwaka wa tatu.

https://p.dw.com/p/4cq43
Vita vya Ukraine | Miaka miwili tangu vita vilipozuka | Kyiv
Bendera za Ukraine zikiwa zimewekwa kwenye bustani mjini Kyiv Februari 24, 2024 kwa lengo la kuwakumbuka watu waliouawa katika vita, tangu Urusi ilipowavamia miaka miwili iliyopita.Picha: picture alliance/Kyodo

Zelensky amesema kwenye hafla ya kumbukumbu ya miaka miwili ya uvamizi kamili wa Urusi iliyofanyika mjini Kyiv kwamba wamekuwa wakipambana kwa siku 730 na watashinda.

Alikuwa akizungumza sanjari na Mawaziri Wakuu wa Canada, Italia na Ubelgiji pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, waliokwenda Kyiv kuonyesha mshikamano na Ukraine.

Von der Leyen amesema kupitia ukurasa wa X kwamba wanasimama na Ukraine kwa kila hali hivi sasa kuliko wakati wowote ule. Aidha alikabidhi magari 50 kwa jeshi la polisi la Ukraine na mamlaka zake za mahakama.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni anayekaimu uenyekiti wa kundi la mataifa tajiri ulimwenguni, G7 anatarajiwa kuongoza mkutano kwa njia ya mtandao kutokea Kyiv utakaohudhuriwa na Zelensky na viongozi wa Marekani, Italia, Canada, Uingereza, Japan, Ufaransa na Ujerumani.