1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANZIBAR : Kundi la Kiislam lachunguzwa

3 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCwc

Rais Amani Abeid Karume wa Zanzibar amesema hapo jana serikali yake inalifuatilia kundi moja la Kiislam na kuonya dhidi ya harakati zozote zile zisizo halali katika kisiwa hicho chenye utete wa kisiasa.

Kundi hilo la Hizub ut Tahrir limeasisiwa mwaka 1953 na limejizatiti katika kuwaunganisha Waislamu wote katika kisiwa hicho chenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu.

Wanachama wengi wa kundi inaaminika kuwa huwa wa siri baada ya kupigwa marufuku katika nchi kadhaa za Kiarabu ikiwemo Misri na Syria.Pia limepigwa marufuku nchini Urusi.

Karume amewaambia waandishi wa habari kwamba anatambuwa juu ya kuwepo kwa kundi hilo na kwamba wataangalia iwapo makundi ya aina hiyo yanavunja sheria za nchi na ikiwa wanavunja sheria hawatosita kuchukuwa hatua kwa kuwa wana sheria mkononi mwao.

Mapema wiki hii kundi hilo lilipachika makaratasi kwenye maduka na sokoni likitowa wito wa kuunda nchi ya ukhalifa itakayoongozwa na kiongozi mmoja wa Kiislam.

Wakati huo huo Rais huyo wa Zanzibar inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefuta uwezekano wa kuunda serikali ya mseto na chama cha upinzani cha CUF.

Amesema upinzani unapoteza wakati wake kwamba hakuna serikali ya mseto Zanzibar jambo hilo haliko katika sera ya CCM chama tawala nchini Tanzania na wala haliko kwenye ilani yake.