1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Zambia ndio mabingwa wa soka barani Afrika

Zambia imeshinda taji lao la kwanza la mataifa ya bara la Afrika mjini Libreville, mji ambao miaka 19 iliyopita umekuwa eneo la mkasa mbaya zaidi kuwahi kuikumba soka ya nchi hiyo.

Wachezaji wa Zambia wakilibusu kombe

Wachezaji wa Zambia wakilibusu kombe

Chipolopolo jinsi wanavyohamika, waliwalaza Cote d'Ivoire waliokuwa wamepigiwa upatu zaidi kulishinda kombe hilo, magoli 8 – 7 kupitia mikwaju ya penalti baada ya mchuano kukamilika sare ya bila kufungana katika muda wa ziada.

Stoppila Sunzu alifunga penalti ya ushindi baada ya kipa wa Zambia Kennedy Mweene kuipangua penalti ya Kolo Toure naye Gervinho akiifyatua yake juu kabisa ya lango.  Rainford Kalaba alikosa kufunga penalti yake kwa upande wa Zambia. Nahodha wa Cote d'Ivoire Didier Drogba angeipa timu yake ushindi katika dakika ya 70 lakini akashindwa kufunga penalti iliyopaa juu ya goli….

Zambia yawaenzi wenzao waliohusika katika ajali

Wachezaji wa Zambia baada ya penalti ya ushindi

Wachezaji wa Zambia baada ya penalti ya ushindi

Kulikuwa na mbwembwe za kila aina uwanjani wakati nahodha wa Zambia Christopher Katongo alipolipokea kombe kutoka kwa Marais wenyeji wa dimba hilo Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta na Ali Bongo Ondimba wa Gabon. Zambia walionekana kutimiza ahadi yao ya kuwaenzi wenzao walioangamia kwenye ajali ya ndege mnamo mwaka wa 1993 katika pwani ya Libreville.

Wageni mashuhuri wakiwemo Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA Sepp Blatter, Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya UEFA Michel Plattini, gwiji wa soka Pele, Rais wa Zambia Michael Satan na mwenzake wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara walikuwa katika uwanja wa Stade de l'Amitie.

Kinyang'anyiro kijacho kitaandaliwa nchini Afrika kusini mwaka ujao 2013 badala ya Misri kutokana na mzozo unaoshuhudiwa nchini humo. Shirikisho la CAF liliamua kupanga ratiba mpya ya dimba hilo ili kutovuruga mechi za kombe la dunia na zile za Euro.

Mashabiki wachache walijitokeza katika baadhi ya mechi

Uwanja wa Estadio de Bata nchini Guinea ya Ikweta

Uwanja wa Estadio de Bata nchini Guinea ya Ikweta

Katika dimba hilo suala la viwanja vitupu katika baadhi ya mechi halikuepukika. Lakini Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika - CAF Issa Hayatou alilitetea shirikisho hilo akisema hawana mamlaka yoyote ya kuwaamuru mashabiki kuhudhuria mechi. Mashabiki wengi walifurika tu viwanjani wakati timu mwenyeji za Gabon na Guinea ya Ikweta zilikuwa zikicheza na kwingineko picha ilikuwa tofauti. Kwa mfano kulikuwa na mashabiki 132 waliohudhuria mchuano baina ya Sudan na Burkina Faso katika uwanja wa Bata ambao una uwezo wa kuwa na mashabiki 30,000.

Tukierejea hapa Ujerumani ni kuwa ligi ya soka Bundesliga inatishia kuwa mbio za farasi watatu baada ya timu za Borussia Dortmund, Bayern Munich na Borussia Moenchengladbach kushinda mechi zao, nayo Schalke 04 ikiteleza.

Wakati huo huo kocha mwengine alipigwa kalamu baada ya klabu ya Hertha Berlin kuduwazwa na VfB Stuttgart kwa magoli matano kwa nunge. Huo ndio ulikuwa mchuano wa mwisho wake kocha Michael Skibbe ambaye alipewa kazi hiyo baada ya kurejea kwa awamu ya pili kuchukua nafasi ya Markus Babbel ambaye pia alionyeshwa mlango.

Bundesliga sasa ni ya farasi watatu kileleni?

Mshambulizi wa Dortmund Shinji Kagawa akisherekea bao lake dhidi ya Bayer Leverkusen

Mshambulizi wa Dortmund Shinji Kagawa akisherekea bao lake dhidi ya Bayer Leverkusen

Dortmund waliwashinda Bayer Leverkusen goli moja wa sifuri na hivyo wanaongoza jedwali na faida ya pointi mbili. Bayern nao waliwazidi nguvu Kaiserslautern kwa kuwapa kichapo cha mabao mawili bila jawabu. Borussia Moenchengladbach waliwanyamazisha Schalke 04 kwa mabao matatu kwa nunge na kuwafanya kuwa nyuma ya Bayern na tofauti ya ponti moja.

Kwingineko barani Ulaya mabao matatu yake Christiano Ronaldo yaliwasaidia Real Madrid kuushinda mchuano wa jana nyumbani dhidi ya Levante. Ushindi huo wa mabao manne kwa mawili uliwapa Real uongozi wa jedwali na faida ya pointi kumi mbele ya mahasimu wao Barcelona, ambao walilazwa na Osasuna mabao matatu kwa mawili.

Nchini Uingereza Manchester United iliwafunga Liverpool mabao mawili kwa moja lakini mchuano huo utakumbukwa kwa Luis Suarez kukataa kumsalimu mkononi Patrice Evra. Suarez alipatikana na hatia ya kumtolea Evra matamashi ya kibaguzi. Hata hivyo mahasimu wa United Manchester City walirejea kileleni mwa jedwali wakiwa na faida ya pointi mbili baada ya kuishinda Aston Villa bao moja kwa nunge. Nambari tatu Tottenham Hotspurs walimwonesha Harry Redknapp kuwa wanamhitaji zaidi katika timu hiyo badala ya kuchukua nafasi ya kuwa kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, kwa kuwasambaratisha Newcastle magoli matano kwa nunge. Chelsea ilishindwa mbili kwa sifuri na Everton huku Arsenal ikiwashinda Sunderland magoli mawili kwa moja.

Awamu ya 16 ya ligi ya mabingwa yarejea

Nembo ya ligi ya mabingwa UEFA

Nembo ya ligi ya mabingwa UEFA

Na mechi za mkondo wa kwanza wa awamu ya 16 ya ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA zinarejea hapo kesho Jumanne, ambapo Olympique Lyon itakabana koo na Apoel Nocosia. Bayer Leverkusen itawakaribisha Barcelona. Siku ya Jumatano Zenit St Petersburg itachuana na Benfica huku AC Milan ikiumiza nyasi na Arsenal.

Katika riadha Mkenya Charles Ndirangu mwenye makao yake nchini Japan aliwaongoza Wakenya wengine katika nafasi ya kwanza, pili na tatu katika mbio za nyika za kimataifa kilomita 12 kwa wanaume mjini Chiba. Ndirangu alitumia muda wa dakika 34 sekunde 59, na kumshinda Martin Mathathi aliyemaliza kwa dakika 35 sekunde 09 na John Gathaiya aliyetimka kwa muda wa 35 sekunde 38.

Katika kitengo cha wanawake kilomita nane Mkenya Susan Wairimu alishinda akifuatwa na Mkenya mwengine Grace Kimanzi na nafasi ya tatu ikanyakuliwa na Megumi Kinukawa kutoka Japan.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/dpa

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed