1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watoto laki tatu wahamiaji wanasafiri wenyewe

Caro Robi
18 Mei 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limesema zaidi ya watoto laki tatu wahamiaji wamesafiri bila ya kuandamana na watu wazima katika mazingira yanayohatarisha maisha yao

https://p.dw.com/p/2d96L
Griechenland Flüchtlingskinder im Ritsona-Camp
Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

UNICEF imesema idadi kubwa ya watoto wakiwa pekee yao wanasafiri kutoka eneo moja hadi jingine aidha kutoroka vita vya Syria, magenge ya wahalifu Amerika Kuisni, mizozo na baa la njaa.

Kiasi ya watoto laki mbili waliomba hifadhi katika mataifa 80 kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana na wengine laki moja walizuiwa katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Mratibu maalumu wa UNICEF kuhusu wakimbizi na wahamiaji barani Ulaya Afshan Khan amesema hilo linawatia wasiwasi mkubwa.

Wengi wa watoto wanatoroka vita na dhiki

Miongoni mwa watoto hao laki tatu, 170,000 walitafuta hifadhi barani Ulaya kati ya mwaka 2015 hadi 2016 baada ya kusafiri kupitia bahari ya Mediterrania ambapo takriban watoto 700 walikufa kufa maji mwaka jana wengi wao kutoka Eritrea, Gambia, Nigeria, Misri na Guinea.

EU Türkei Migration Flüchtlingsabkommen
Watoto wakimbizi wa Syria wakiwa kambini UturukiPicha: DW/D. Cupolo

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema thuluthi moja ya waathiriwa wa biashara haramu ya ulanguzi wa watu duniani ni watoto ambao hukumbwa na ghasia, unyanyasaji wa kingono, kutumikishwa, kunyofolewa baadhi ya sehemu zao za mwili ili kuuzwa na madhila mengine.

Kati ya watoto watano wahamiaji au wakimbizi, watatu wanaotokea nchi za Amerika ya Kusini na Carribean wamekuwa waathiriwa wa biashara haramu ya ulanguzi wa watu,wengi wao wakiuzwa kama watumwa wa ngono.

Mkurugenzi wa UNICEF wa kanda ya Amerika ya Kusini Maria Cristian Perceval amesema biashara ya kuwatumia wasichana na wavulana wadogo kingono imekuwa biashara kubwa na kuongeza wanaoawasaidia watoto hao wakiwa safarini huwabaka, kuwapiga na kuwataka kulipa ili waendelee na safari zao.

Libya imekuwa soko la utumwa

Mmoja wa watoto hao Mary kutoka Nigeria alikwama Libya akielekea Italia kwa miezi mitatu ambako alibakwa mara kadhaa na mfanyabiashara wa kusafirisha wahamiaji ambaye alimtishia kuwa hatomfikisha Ulaya iwapo hatolala naye.

Mittelmeer Flüchtlingsboot
Boti lililojaa wahamiaji na wakimbizi likitokea LibyaPicha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Mtoto mwingine kwa jina Aimamo amesema yeye na pacha wake walilazimishwa kufanya kazi katika shamba moja Libya kwa miezi miwili ili kuwalipa waliowasafirisha kufika huko akiongeza ukijaribu kutoroka wanakuuawa kwa kukupiga risasi,ukiacha kufanya kazi wanakupiga na baada ya kazi wanakufungia.

UNICEF imelitaka kundi la nchi saba tajiri zaidi duniani G7 linalokutana Italia baadaye mwezi huu kuangazia suala hilo kwa kuahidi kuwalinda zaidi watoto, kuimarisha juhudi za kuziweka pamoja familia, watoto hao kupata elimuu na huduma za afya na pia kushughulikia kinachosababisha wimbi kubwa la wahamiaji la wakimbizi, kukomesha chuki dhidi ya wageni na ubaguzi katika nchi wanazopitia na kufikia.

Mwandishi: Caro Robi/Thomson Reuters/dpa/afp

Mhariri: Yusra Buwayhid