1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen: Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh auawa

4 Desemba 2017

Wizara ya ndani ya Yemen imetangaza kuuawa kwa Ali Abdullah Saleh kupitia kituo rasmi cha televisheni cha Al-Masirah

https://p.dw.com/p/2ojrs
Jemen Ali Abdullah Saleh
Picha: picture alliance/AP Photo/Muhammed Muheisen

Rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh ameuawa. Taarifa hiyo imethibitishwa na wizara ya ndani  inayodhibitiwa na waasi  wa kihouthi nchini Yemen baada ya kuibuka video iliyoonekana ikiionesha maiti ya Abdullah Saleh. Haya yanajiri huku kukiwa na mapigano makali katika mji wa Sanaa kufuatia kusambaratika kwa muungano wa waasi.

Chama cha rais huyo wa zamani GPC kimethibitisha kuuawa kwake. Kiongozi wa chama hicho Faiqa al-Sayyid amewalaumu waasi wa Kihouthi kwa kumuua Saleh. Faiqa ameeleza kuwa Saleh pamoja na wakuu wengine wa chama waliuawa walipokuwa wakikimbia mji wa Sanaa unaodhibitiwa na waasi wakielekea maeneo ambayo yanadhibitiwa na vikosi vitiifu kwake.

Kwa mujibu wa duru ya kijeshi, wanamgambo wa Kihouthi walisimamisha msafara wa magari 4 ya Saleh takriban kilomita 40 kusini mwa Sanaa, wakampiga risasi Saleh na kumuua. Aidha walimuua Katibu Mkuu wa chama Arif al-Zouka na naibu wake Yasir al-Awadi.

Baadhi ya waliokuwa wakimuunga mkono Saleh Abdullah
Baadhi ya waliokuwa wakimuunga mkono Saleh AbdullahPicha: picture-alliance/AA/M. Hamoud

Wizara ya ndani ya Yemen imetangaza kupitia kituo rasmi cha televisheni cha Al-Masirah kwamba mzozo wa wanamgambo umemalizika kufuatia kuuawa kwa Saleh ambaye alikuwa kiongozi wao pamoja na wafuasi wake kadhaa waliokuwa na silaha.

Tangazo la kuuawa kwa Abdullah Saleh limejiri baada ya video iliyoonesha kile kilichoaminika kuwa maiti ya Saleh iliyofunikwa kwenye blanketi huku kichwa kikiwa na jeraha baya, kuanza kusambaa katika mitandao ya kijamii. Video hiyo haijathibitishwa

Kusambaratika kwa muungano wa waasi

Akitangaza taarifa hiyo, mtangazaji wa televisheni ya Al-Masirah amesoma: "Wizara ya ndani inatangaza mwisho wa waasi kwa kuchukua udhibiti wa maeneo yao na kurejesha usalama katika mji wa Sanaa, viunga vyake na katika mikoa yote. Pia inatangaza kuuawa kwa kiongozi wa wasaliti na baadhi ya wapambe wake."

Mapema leo, waasi wa Kishia waliripua nyumba ya Saleh mjini Sanaa, muda mfupi baada ya kuivamia. Wahouthi pia walidai kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa ambayo vikosi vitiifu kwa Saleh vilikuwa vikidhibiti na kuongeza kuwa mamia kadhaa ya wanamgambo hao walijisalimisha.

Moshi ukifuka katika mji wa Sanaa kufuatia mapigano kati ya wapiganaji wa Kihouthi na vikosi vitiifu kwa aliyekuwa rais wa zamani wa Yemen Abdullah Saleh
Moshi ukifuka katika mji wa Sanaa kufuatia mapigano kati ya wapiganaji wa Kihouthi na vikosi vitiifu kwa aliyekuwa rais wa zamani wa Yemen Abdullah SalehPicha: Reuters/M. al-Sayaghi

Kulingana na Kamati kuu ya shirika la Msalaba Mwekundu , watu 125 wameuawa na 238 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya hivi karibuni.

Saleh alitawala Yemen kwa miongo mitatu

Mnamo Jumamosi, Saleh alitangaza mwisho wa ushirikiano wake na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, na ambao ametawala nao kwa pamoja mji mkuu wa Sanaa kwa miaka mitatu.

Saleh aliyekuwa na umri wa miaka 75, na mwenye nguvu alitawala Yemen kwa zaidi ya miongo mitatu hadi alipoondolewa kufuatia shinikizo la kisiasa mwaka 2012.

Lakini alisalia nchini humo na kuendelea kuwa na ushawishi wa mamlaka kwa mlango wa nyuma. Licha kwamba aliwahi kupambana na wanamgambo wa Wahouthi mara kadhaa, mnamo 2014 vikosi vyake vilishirikiana na Wahouthi. Muungano huo wa waasi uligawika  wiki iliyopita na kusababisha mapigano makali kati ya Wahouthi na vikosi vya Saleh.

Mapigano kati ya pande hizo mbili yalianza Jumatano wiki iliyopita  wakati wanamgambo wa Kihuthi walipovamia msikiti muhimu wa Sana'a unaodhibitiwa na vikosi vitiifu kwa Saleh. Pande zote mbili zimekuwa zikilaumiana kufuatia vita hivyo.

Ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimekuwa zikifanya mashambulizi katika ngome za waasi wa Kihouthi.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Yusuf Saumu