1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

YAOUNDE:Mvua yafanyakazi ya uokozi wa ajali ya ndege ya Kenya kuwa ngumu

6 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC4R

Waokoaji wanajiandaa asubuhi hii kuendelea na kazi ya kutafuta mabaki ya ndege ya shirika la ndege la Kenya iliyoanguka mapema jana huko Cameroon ikiwa na abiria 114.

Mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha imewazuia waokoaji wanaoshirikiana na wanavijiji kuendelea na kazi hiyo.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 ilipoteza mawasiliano hapo jana muda mfupi baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Douala nchini Kenya kueleka Nairobi.Inahofiwa kuwa hali mbaya ya hewa huenda ikawa chanzo cha ajali hiyo.

Wakaazi wa mji wa Lolodorf uliyoko kiasi cha kilomita 100 kusini magharibi mwa Younde, wamesema kuwa walisikia mshindo mkubwa wakati ndege hiyo ilipoanguka kwenye msitu uliyoshikamana wa eneo hilo.

Helikopta za kijeshi zikishirikiana na wanavijiji wanaotumia baiskeli wamekuwa wakitafuta mabaki ya ndege hiyo, lakini hata hivyo mvua kubwa zinazonyesha zimewazuia.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya amesema kuwa ametuma ujumbe wa ngazi ya juu kutoka serikalini ukiongozwa na waziri wa usafiri Chirau Ali Mwakwere kusaidiana na mamlaka za Cameroon kutafuta chanzo cha ajali hiyo.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Kenya, Titus Naikuni alisema kuwa Serikali ya Kenya ilikuwa imeanzisha kazi ya uokoaji.

Kituo cha jeshi la Ufaransa kilichoko nchini Gabon kimetoa Helkopta moja kusaidia kazi hiyo.

Serikali ya Cameroon imeweka vituo viwili vya dharura katika miji ya Douala na Younde ili kushirikiana katika kazi ya uokoaji

Shirika hilo la ndege la Ndege la Kenya limesema kuwa abiria wanaohisiwa kufa kwenye ajali hiyo ni wa kutoka nchi zipatazo ishirini, akiwemo mmoja kutoka Tanzania.

Wengine ni kutoka, afrika, kusini, Cameroon, India, Ghana, Mali, Togo, Nigeria, Uingereza, Kongo Kinshasa, Kongo Brazaville, Swaziland, Komoro, Bukina Faso na Marekani.

Halikadhalika walikuwa abiria kutoka Misri, Mauritius, Senegal,Niger na China.

Wakati huo huo Shirika la soka barani afrika limesema kuwa waamuzi watatu wa mpira kutoka Cameroon ni miongoni mwa abiria waliyokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Waamuzi hao walikuwa wakielekea Kinshasa kupitia Nairobi kwenda kuchezesha mechi za shirikisho hilo kati ya timu ya Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo na timu kutoka Zimbabwe.

Ndege hiyo ni mpya na ilinunuliwa miezi sita iliyopita.Shirika la ndege la kenya lina ndege nyingine za aina hiyo mbili na maafisa wake hawajaamua kama wazisimamishe au la.