Yaliyomo magazetini hii leo | Magazetini | DW | 28.11.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Yaliyomo magazetini hii leo

Mkutano mkuu wa CDU na kuvunjika mazungumzo kati ya Brussels na Uturuki ndizo mada zilizomulikwa na wahariri wa Ujerumani

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika zaidi juu ya kushindwa mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki kuhusiana na suala la Cyprus na mvutano kuhusu mkondo unaobidi kufuatwa na chama cha Christian Democratic-CDU kinachoendelea na mkutano wake mkuu huko Dresden.

Kuhusu mkondo wa kufuatwa na chama cha CDU gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

„Hata kiwezekanacho kinahitahji kufikiriwa“-alisema kansela Angela Merkel kwenye mkutano huo mkuu.Lakini hakuna chochote cha kuwazia kilichokuwemo katika hotuba yake.Mkondo bayana wa siasa ya mambo ya nchi za nje ya Merkel umefunika kikamilifu siasa ya mambo ya ndani.Anapigia upatu mageuzi ya mfumo huru wa kiuchumi unaotilia maanani masilahi ya kijamii na kutaja kama juhudi zitakazoamua juu ya mustakbal wa nchi yetu-hasemi lakini vipi.Mageuzi yanahitaji msimamo, na huo pia hanao .“

Maoni sawa na hayo yametolewa na gazeti la mjini Berlin TAGESZEITUNG.TAZ linaandika:

„Wana Christian Democrats hawajui tena kipi kinaweza kutokana na uchumi wa soko huru katika ulimwengu wa utandawazi,na haki inaweza kupatikana kwa namna gani, kwa kuzidisha mashindano ya kibiashara,kwa kuzidisha marupu rupu yanayotolewa na serikali au kwa kuimarisha mfumo wa elimu.Mjadala kuhusu hofu za wananchi uliozushwa na Jürgen Rüttgers si chochote chengine,ni ukosefu wa muongozo na wala si sehemu ya ufumbuzi.“

Gazeti la Handelsblatt linajishughulisha na mapendekezo ya waziri mkuu wa jimbo la Nordrhein Westfalia-Jürgen Ruttgers na kuandika:

„Mnamo miezi ya hivi karibuni,hata mwenye kuzungumzia dhamiri zake mwenyewe,anatajwa kua „mwanamapinduzi.Hayo hayo ndiyo aliyoyafuata Jürgen Rüttgers ili kupanda daraja ya umaarufu katika siasa za shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.Mapendekezo yake kutaka pawepo muda tofauti wa malipo ya fedha za ukosefu wa ajira si mageni katika mkakati wa CDU.Na wala si dhambi pia la kisiasa seuze kama litaifanya serikali ifilisike.Chanzo halisi lakini cha mvutano aliouchochea na kuugubika mkutano mkuu wa chama cha CDU mjini Dresden,kinakutikana katika ile hali kwamba CDU haijui kipi cha kufanya mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani serikali ya muungano wa vyama vikuu.“

Gazeti la WESTFÄLISCHE RUNDSCHAU linaandika:

„Rüttgers amezungumzia kile ambacho tokea hapo ni sehemu ya mkakati wa CDU:“Bidii zilete tija hata wakati mtu anapokua hana ajira.“Hakujakua na namna nyengine bora zaidi ya kutathmini misingi ya mshikamano wa kijamii.Hata kama Jürgen Rüttgers atataka kulitaja pigo la kupoteza kura kama matokeo ya mvutano wa mkondo wa aina gani ufuatwe ndani ya CDU,ukweli lakini ni kwamba wana CDU walitaka kumkatizia kiu cha kujipendekeza.“

Mada nyengine iliyochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani imehusu kushindwa mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki-mzizi wa fitina ukisalia kua suala la kisiwa kilichogawika cha Cyprus.

Gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND ,linahisi mzozo huu una chanzo na Uturuki sio sababu.Gazeti limekumbusha walikua Wacyprus wenye asili ya Ugiriki waliopinga kura ya maoni ya mwaka 2004 kama kisiwa cha Cypurus kiungane tena-wakiamini wakiwa wanachama wa Umoja wa Ulaya,hawatakua na hasara.Uturuki lakini bila ya idhini ya wa- Cyprus wenye asili ya Ugiriki haiwezi kuwa mwanachama.Kwa hivyo si haki na wala si sawa kusema mazungumzo yamevunjika kwasababu ya suala la Cyprus.

 • Tarehe 28.11.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUL
 • Tarehe 28.11.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUL