1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Yaliyochambuliwa magazetini hii leo

Angela merkel na serikali yake mwaka mmoja madarakani na mauwaji nchini LIbnan ndizo mada zilizochambuliwa magazetini hii leo

Mwaka mmoja tangu serikali ya muungano wa vyama vikuu kuingia madarakani mjini Berlin,na hali nchini Libnan ndizo mada zilizomulikwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Serikali ya muungano wa vyama vikuu inayoongozwa na kansela Angela Merkel imetathmini mwaka mmoja tangu walipoingia madarakani.Katika mjadala wa bunge la shirikisho mjini Berlin,kansela Angela Merkel amekumbusha uchumi wa Ujerumani umeanza kunawiri baada ya kuzorota kwa miaka kadhaa.Kansela ameahidi wataendelea na mkondo wa mageuzi.Lakini matumani hayo mema ya kansela Angela Merkel ,wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanayapima kwa jicho la tahadhari.

Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock linaandika:

„Kulikua na hata mauwa aliyotunukiwa kansela ambae baada ya kutoa ahadi kubwa kubwa za kisiasa,naiwe kuhusu sheria za usawa wa jinsia,malipo ya wazee au mageuzi ya mfumo wa afya, na uhuru mkubwa zaidi ,amerejea katika mtindo ule ule wa ufumbuzi wa dondoo.Makubwa aliyoyaahidi bado yanamsubiri.“

Gazeti la mjini Cologne,KÖLNISCHE RUNDSCHAU linaonya dhidi ya watu kujipa matumaini makubwa na kuandika:

„Katika mjadala wa bajeti katika bunge la shirikisho Bundestag serikali ya muungano wa vyama vikuu imeonekana kwa upande mmoja kana kwamba inajinata kwa yale yaliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja madarakani na kwa upande wa pili lakini imejitokeza kama imepwaya.Hakuna sababu lakini ya kujihisi hivyo.Kwasababu yaliyotiwa njiani bado hayawezi kusifiwa kama ufanisi na hata kilichoshindikana sio sababu kwa serikali kukata tamaa.“

Gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG la mjini Gera linahisi chama cha CDU hakina msimamo mmoja.Gazeti linaandika:

„Ingawa dondoo hujaza mtungi,lakini bado si dhahiri Merkel anafuata mkondo gani.Mijadala ndani ya chama cha Christian Democratic kuhusu nani anastahiki kua naibu mwenyekiti wa chama,kwa muda gani watu wasiokua na kazi waendelee kusaidiwa kifedha na serikali au sera za jamii ziwe za aina gani,mijadala hiyo itakifikisha wapi chama hicho?Kwamba katika serikali kuu ya muungano kansela anasimamia tuu badala ya kuongoza pengine ndio sababu ya hali hiyo,lakini CDU wanaweza pia kumpatia muongozo Angela Merkel.

Tuiingilie mada ya pili magazetini.Hali bado ni ya wasi wasi nchini LIbnan baada ya shambulio lililogharimu maisha ya waziri wa viwanda Pierre Gemajel.Wanasiasa kadhaa wanatahadharisha dhidi ya kugawika Libnan.Hata wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameingiwa na hofu.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linahisi pengine Syria iko nyuma ya kuuliwa wanasiasa wengi wanaoipinga nchi hiyo jirani.

Gazeti linaandika:

„Uchunguzi ulioongozwa na Umoja wa mataifa unaashiria uwezekano wa kuhusika Syria na mauwaji nchini :Libnan na kuwagonganisha vichwa wananchi,hata kama serikali ya Damascus inakanusha.Wapinzani wa Syria mjini Beirut wameonyesha mshikamano kufuatia mauwaji ya hivi karibuni,lakini wakati huo huo mauwaji hayo hayo yamezidisha ufa katika jamii na kutishia kuigawa nchi hiyo.

Hoja sawa na hizo za kugawika Libnan zimechambuliwa pia na gazeti la LANDESZEITUNG la mjini Lüneburg linalofika hadi ya kuhofia vita vya wenyewe kwa wenyewe..

 • Tarehe 23.11.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUN
 • Tarehe 23.11.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHUN