1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wolfsburg yajihakikishia kandanda la Ulaya msimu ujao

11 Mei 2015

VLF Wolfsburg imeishinda SC Parderborn kwa mabao 3-1 na kujihakikishia nafasi ya Champions League msimu ujao baada ya kujiimarisha katika nafasi ya pili ya Bundesliga wakati zimebaki mechi mbili

https://p.dw.com/p/1FOGc
Fußball Bundesliga 32. Spieltag SC Paderborn vs. VfL Wolfsburg
Picha: picture alliance/Simka/CITYPRESS 24

Bayern Munich ambayo tayari imekwisha jihakikishia ubingwa msimu huu, ilipoteza mchezo wake kwa bao 1-0 dhidi ya Augsburg ikiwa ni kipigo chake cha nne mfululizo katika mashindano yote inayoshiriki msimu huu wakati kikosi hicho cha Pep Guardiola kikijitayarisha kwa mpambano dhidi ya Barcelona katika mchezo wao wa nusu fainali mkondo wa pili kesho Jumanne.

Borussia Moenchengladbach, inashikilia nafasi ya tatu , na imesogea karibu na kushiriki kwa mara ya kwanza katika awamu ya makundi ya Champions League baada ya kuwaangusha kwa kishindo mahasimu wao Bayer Leverkusen kwa mabao 3-0 Jumamosi jioni. Nini sababu ya Gladbach kuwa moto wa kuotea mbali msimu huu, anaelezea mchezaji wa kati Christoph Kramer ambaye anarejea Leverkusen msimu ujao.

Bundesliga Gladbach gegen Leverkusen
Gladbach iko katika nafasi nzuri ya kufuzu katika Champions LeaguePicha: M. Hangst/Bongarts/Getty Images

Timu zilizoko katika hatari ya kushuka daraja , zinapambana kufa na kupona kuweza kujinasua kutoka katika hali hiyo. VFB Stuttgart ikiwa ya mwisho kabisa katika msimamo wa ligi, imejitutumua siku ya Jumamosi na kupata ushindi muhimu unaoiweka timu hiyo katika matumaini ya kuokoka kutoka janga hilo, baada ya kuishinda Mainz 05 kwa mabao 2-0. Huu ni ushindi muhimu kwa Stuttgart ambayo iko mkiani kabisa mwa ligi, ikiwa na pointi 30 kibindoni, kama anavyosema mshambuliaji wa timu hiyo Daniel Didavi.

Hamburg SV ikiwa na pointi 32 iko nafasi ya 14 nafasi mbili juu kuliko timu zilizoko katika nafasi ya kushuka daraja. Lakini nafasi hiyo haina uhakika kwamba Hamburg imejitoa katika wasi wasi wa kushuka daraja, kwani imepishana pointi moja tu na timu tatu za chini zikiwa na pointi 31. SC Freiburg , Hannover 96, SC Parderborn zote zina uwezo wa kujinasua kutoka janga hilo la kushuka daraja iwapo zitashinda michezo yake miwili iliyobaki. Stuttgart ikiwa na pointi 30 pia inaweza kujinasua kutoka janga hilo. Ni timu ipi inaweza kushuka daraja msimu huu , hilo ni swali na kungoja na kuona.

Borussia Dortmund inasogelea nafasi ya kucheza katika ligi ya Ulaya , Europa League ikiwa katika nafasi ya 7 , na pointi mbili nyuma ya mahasimu wao wakubwa Schalke 04, ambao jana Jumapili walipata pigo , baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya FC Kolon. Kocha wa Borussia Dortmund Juergen Klopp anasema amefarijika sana na matokeo ya timu yake hivi karibuni.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae / ape / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga