Wolfowitz atafuta njia muafaka ya kujiuzulu. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wolfowitz atafuta njia muafaka ya kujiuzulu.

Uungaji mkono wa hivi karibuni wa Ikulu ya Marekani kwa rais wa benki kuu ya dunia Paul Wolfowitz ambaye amezingirwa na matatizo katika wadhifa wake, licha ya matokeo ya uchunguzi uliomo katika ripoti ya ndani ya taasisi hiyo ambayo inasema kuwa amekiuka sheria na maadili ya taasisi , unasababisha jukumu la Marekani katika kuendesha benki hiyo kuwa katika uchunguzi kwamba unakwenda kinyume na njia za kidemokrasi , wakati huo huo kukiwa na miito kadha ya kutaka Marekani kupunguza nguvu zake katika taasisi hiyo.

Wolfowitz, akitafakari jinsi ya kujinasua kutoka kashfa inayomhusisha yeye na mpenzi wake.

Wolfowitz, akitafakari jinsi ya kujinasua kutoka kashfa inayomhusisha yeye na mpenzi wake.

Rais wa benki kuu ya dunia ambaye hivi sasa anakabiliwa na tuhuma za kashfa dhidi yake Paul Wolfowitz amekuwa akitafuta njia muafaka ya kujitoa kutoka katika kashfa hiyo inayohusu malipo ya mshahara kwa mpenzi wake wa kike , wakati viongozi wa benki hiyo wanajitayarisha kwa ajili ya mazungumzo zaidi kuhusiana na mustakabali wake leo Alhamis.

Wolfowitz ambaye ni mshirika wa karibu na wa muda mrefu wa rais wa Marekani George W. Bush, aliripotiwa kuwa tayari kujiuzulu pale tu benki hiyo itakapochukua kiasi cha lawama kutokana na ushauri wake wa kukanganya kuhusiana na ongezeko la utata la mshahara aliloshauri kwa ajili ya mpenzi wake huyo.

Mataifa ya Ulaya yamekuwa yakitoa mbinyo mkali kwa naibu waziri huyo wa zamani wa ulinzi wa Marekani kuondoka madarakani kutoka katika taasisi hiyo yenye wanachama 185 na hata uungaji mkono wa Ikulu ya Marekani umepungua katika siku za hivi karibuni wakati utata juu ya kashfa hiyo ukiongezeka.

Suala hapa ni jukumu la Wolfowitz katika kupanga ongezeko kubwa la mshahara na uhamisho kwa mpenzi wake na mfanyakazi mwezie katika benki hiyo, Shaha Riza, baada ya kuchukua wadhifa huo mwaka 2005.

Ripoti inayomchafua kabisa iliyotolewa na jopo la uchunguzi ndani ya benki hiyo wiki hii imegundua kuwa Wolfowitz amekiuka sheria za benki katika kupanga mpango huo kwa Riza, lakini pia imesema ripoti hiyo kuwa benki imempa maelekezo yasiyoeleweka juu ya suala hilo.

Duru karibu na benki hiyo zimesema jana Jumatano kuwa makubaliano yanayofikiriwa, yatalazimu benki hiyo kutambua kuwa , ingeweza kumpatia muongozo mzuri zaidi juu ya kuepuka hali ya mzozo wa kimaslahi.

Wakili wa Wolfowitz Robert Bennet , pamoja na maafisa wa benki ya dunia walifanya majadiliano ambayo yamefikia katika kiwango cha upeo wa juu, imeripoti televisheni ya CNBC.

Utawala wa rais Bush umekuwa ukimkingia kifua Wolfowitz kwa nguvu zote, ikiwa ni mmoja kati ya wasanifu wakuu wa vita vya Iraq, licha ya miito kadha kutoka mataifa ya Ulaya kumtaka ajiuzulu.

Katika wizara ya mambo ya nje nchini Marekani, msemaji wa wizara hiyo Tom Casey amesema kuwa benki hiyo ni taasisi kubwa kuliko mtu yeyote binafsi, waliopita, wa hivi sasa ama watakaokuja.

Wolfowitz amekuwa akiendesha benki hiyo kwa muda wa miaka miwili iliyopita. Na siku ya Jumanne aliwaomba wakurugenzi wa benki kumwacha katika wadhifa huo , ambapo ametoa ahadi ya kupambana na ulaji rushwa.

Nimesema kuwa siepuki lawama kuhusu suala hili, Wolfowitz amesema kuhusiana kashfa hiyo inayomhusisha Riza, ambaye amekuwa akijipatia mshahara wa dola 200,000 kwa mwaka baada ya kuhamishiwa katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani akiwa , bado katika orodha ya malipo kutoka benki kuu ya dunia.

Afisa mmoja wa Marekani amenukuliwa na gazeti la Washington Post jana Jumatano akisema kuwa Marekani na mataifa ya Ulaya yanafikiria kupata makubaliano ambayo Wolfowitz atajiuzulu baada ya kusafishwa jina lake , kwamba hakufanya kosa.

 • Tarehe 17.05.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHEE
 • Tarehe 17.05.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHEE

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com