1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito kupiga marufuku mabomu ya mtawanyo

P.Martin21 Februari 2007

Mabomu ya mtawanyo yaliotumiwa Irak na Afghanistan,hasa yaliwavutia watoto kwa sababu ya ile rangi ya manjano ya mabomu hayo.

https://p.dw.com/p/CHJc

Watoto hawafahamu kuwa hayo ni mabomu yanayongojea kuripuka na huwa wahanga wa silaha hizo.Si rangi tu inayobababisha,kwani mabomu hayo ya mtawanyo hufanana pia na vile vifurushi vya chakula vinavyotolewa na Marekani,kwa hivyo hata watu wazima hubabaika na kosa hilo hugharimu maisha yao.

Wanaharakati na mashirika yasio ya kiserikali yanayogombea haki za binadamu na ambao tangu miaka,wanataka mabomu hayo yapigwe marufuku,hii leo wanakutana katika mji mkuu wa Norway,Oslo. Serikali ya Norway,inazindua ushirikiano mpya kwa lengo la kuzuia utumiaji wa mabomu ya mtawanyo. Wakati huo huo,mashirika ya Kijerumani yasio ya kiserikali yanasema,mkutano huo wa Oslo uweke msingi mpya wa sheria ya kimataifa,kupiga marufuku mabomu ya mtawanyo.

Kiongozi wa muungano wa mashirika hayo,bwana Thomas Küchenmeister amesema,hadi hivi sasa madhara yanayosababishwa na silaha hizo hayakutiwa sana maanani.Lakini mabomu ya mtawanyo ni kama mabomu yaliotegwa ardhini.Amesema,sababu ya kulinganisha mabomu ya mtawanyo na yale yanayotegwa ardhini ni kwamba baadhi kubwa ya mabomu ya mtawanyo yanayokosa kuripuka,hubakia kwenye ardhi na huripuka yanapoguswa au kukanyagwa na mtu.Kwa hivyo ni sawa na mabomu yaliotegwa ardhini na ni hatari sana.

Mabomu ya mtawanyo yamewahi kutumiwa kama silaha nchini Laos,Sudan,Afghanistan na hata Irak.Katika mwaka 2001,Marekani iliangusha zaidi ya mabomu 1,200 ya aina hiyo nchini Afghanistan na asilimia 10 ya mabomu hayo hayakuripuka.Na mwaka jana, kufuatia mashambulizi ya Israel,theluthi moja ya ardhi ya kilimo,kusini mwa Lebanon,ilichafuliwa kwa mabomu ya mtawanyo.

Mabomu ya aina hiyo si hatari kwa muda mfupi tu kwa miili na maisha ya wakaazi,bali ni hatari ya muda mrefu pia.Kama kiongozi wa chama cha Kijani cha Ujerumani Claudia Roth anavyosema,”

“Utumiaji wa silaha za aina hiyo,huzuia maendeleo na pia husababisha matatizo katika maendeleo ya eneo zima.Mtu anapofikiria kazi za ukarabati nchini Afghanistan……silaha hizo zimesambaa kwenye ardhi hiyo kama mabomu yanayongojea kuripuka.”

Muungano unaopinga mabomu ya mtawanyo ndio umetoa wito kwa serikali ya Ujerumani,ibadili mkondo wa sera zake za ulinzi,kwani hivi sasa,jeshi la Ujerumani-Bundeswehr- binafsi,lina maelfu kadhaa ya mabomu ya mtawanyo.

Muungano wa mashirika yasio ya kiserikali,unataka kuona hatua thabiti zikichukuliwa ili kukomesha mateso ya binadamu yanayosababishwa na mabomu ya mtawanyo.