1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa kiarabu

15 Februari 2011

Changamoto zinazoikabili Misri ,wimbi la wakimbizi wa Tunisia na mjadala unaoendelea kuhusu kuandikishwa wageni katika jeshi la shirikisho Bundeswehr ndizo mada zilizohanikiza magazetini

https://p.dw.com/p/10HK5
Wakimbizi wa Tunisia kisiwani LampedusaPicha: picture alliance/dpa

Tuanzie Misri ambako wahariri wa magazeti ya Ujerumani bado wanamulika nini kitatokea baada ya Mubarak kuyapa kisogo madaraka.Gazeti la "Döbelner Anzeiger" linaandika:

"Mwito:Mubarak lazma aondoke" ndio chanzo pekee kilichowaunganisha waandamanaji.Vyenzo halisi vilivyowateremsha mamilioni ya wamisri majiani ndio kwanza vinachomoza .Na vyenzo hivyo ni tofauti kabisa.Na zaidi ya yote,vyenzo hivyo si rahisi kuvipatia ufumbuzi kufumba na kufumbua kama ilivyokuwa wakati wa kumshinikiza ang'oke madarakani mtu ambae wote walikuwa wakimtwika jukumu la matatizo yao.Lakini Mubarak hakuitawala Misri peke yake.Ni mfumo wa Mubarak ambao wamisri wengi wanahisi ndio ulioitumbukiza nchi katika hali hii.Mfumo kama huo patahitajika muda mrefu kuweza kuachana nao.Suala ni jee wamisri,baada ya kuonyesha ujasiri mkubwa wataweza pia kuonyesha subira?

Katika Afrika kaskazini na ulimwengu wa kiarabu wimbi la mageuzi ya kidemokrasi limeanzia Tunisia ambako wanamtandao wamefanikiwa kumtimua Zine Al Abidine Ben Ali baada ya miaka 25 madarakani.Mwezi mmoja baadae vijana hao hao wanayatia hatarini maisha yao na kuvuka bahari kuelekea Italy kusaka maisha bora.Wahariri wengi wanaamini huo ni mwanzo tuu wa mkururo wa wahamiaji.Nini la kufanya anajiuliza mhariri wa gazeti la "Bild-Zeitung" la mjini Berlin,na kuendelea:

Kwa mara nyengine tena Ulaya inashuhudia kishindo cha wakimbizi.Maelfu wanaihama Tunisia wakiyatosa maisha yao ndani ya mitumbwi katika bahari iliyochafuka kuelekea Italy.Na huu ni mwanzo tuu.Eneo lote la Afrika Kaskazini limechafuka.Na pasitokee yeyote atakaetwambia eti sisi hatuhisiki.Kama waimla wametimuliwa madarakani leo,wengine wanaweza kufuata ikiwa ulimwengu wa magharibi hautowajibika.Tunabidi tuwasaidie wakaimbizi.Na hili sio suala la kiutu tuu-kipa umbele ni kuhakikisha utulivu katika eneo hilo.Ni sawa kwamba misaada tutabidi tuigharimie.Lakini kila Euro moja ambayo leo hii tutakataa kuitoa,kuna siku itaongezeka mara chungu nzima matatizo yatakapotufikia.Ulimwengu ni mdogo kuweza watu kusema,aha yanayotokea kule,sisi huku hayatuhusu."

NO FLASH Thema Ausländer bei der Bundeswehr
Suala la kujumuishwa wageni katika jeshi la shirikisho BundeswehrPicha: picture alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mipango ya kuajiriwa wageni katika jeshi la shirikisho-Bundeswehr.Gazeti la "Südwestpresse Ulm" linaandika:

Eti kweli wizara ya ulinzi inaweza kumudu kuwaandikisha watu ambao hawana passpoti za Ujerumani kama wanajeshi wanaolipwa mshahara mdogo?Na wapi unakutikana mustakbal wa mwanajeshi anaetakiwa ajiamaini,awe mwerevu na mtu mwenye kutilia maanani tamaduni nyengine anapojikuta akiwajibika nchi za nje?Kwamba jeshi la shirikisho linatakiwa liwe mwajiri anaevutia kuweza kuwavutia wenye vipaji,hakuna anaebisha.Vivutio hivyo ni pamoja na mishahara ya maana,kushughulikiwa wanajeshi na jamaa zao na kadhalika-lakini sio fikra kama hiyo.Na kwa jeshi ambalo linalazimika kupata ridhaa ya bunge,fikra kama hiyo haifai kabisa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/inlandspresse

Mpitiaji:Abdul-Rahman,Mohammed