1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

William Schabas ajiuzulu wadhifa wake

Mjahida3 Februari 2015

Mkuu wa tume ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa inayochunguza mgogoro uliotokea kati ya Israel na Palestina William Schabas, amejiuzulu kufuatia madai ya upendeleo katika kazi yake yaliotolewa na Israel.

https://p.dw.com/p/1EUoh
Mkuu wa tume ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa William Schabas
Mkuu wa tume ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa William SchabasPicha: Simon O’Connor

Katika barua aliyoiandikia kamisheni hiyo, Schabas amesema amejiuzulu haraka iwezekanavyo ili kuzuwiya suala hilo kugubika matayarisho ya ripoti juu ya uchunguzi wao inayotarajiwa kutolewa baadaye mwezi Machi.

Katika barua hiyo, Schabas ameongeza kuwa maoni ya kisheria aliyoyatoa katika kazi aliyoifanya awali kama mshauri wa chama cha ukombozi wa Palestina PLO mwaka wa 2012 hayatofautiani na ushauri aliyowahi kutoa kwa serikali nyengine pamoja na mashirika mengine mengi.

"Maoni yangu juu ya Israel na Palestina na katika masuala mengine mengi yalijulikana na yalikuwa hadharani, hii kazi ya kutetea haki za binaadamu inaonekana kunifanya mimi kulengwa kwa nia ya kunihujumu," alisema William Schabas

Mashambulizi yaliofanywa katika Ukanda wa Gaza
Mashambulizi yaliofanywa katika Ukanda wa GazaPicha: Reuters

Schabas aliteuliwa mwezi Agosti mwaka jana na Mkuu wa Baraza la kutetea haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa kuongoza kundi lililo na wanachama watatu wanaochunguza madai ya uhalifu wa kivita wakati Israel ilipoishambulia Gaza.

Kuondoka kwa Schabas, kunaashiria ugumu uliopo katika uchunguzi unaofanywa na Umoja wa Mataifa wiki kadhaa baada ya waendesha mashtaka wa mahakama ya uhalifu wa kivita ya ICC ilioko mjini the Hague, wakisema kwamba wameanzisha uchunguzi juu ya madai ya ukatili uliofanywa ndani ya ardhi ya Palestina.

Israel yakosoa uteuzi wa William Schabas

Awali Israel ilikosoa uteuzi wa Schabas ikisema kwamba ni mkosoaji mkubwa wa taifa la Israel pamoja na uongozi wake wa sasa. Hata hivyo kamisheni hiyo imemaliza kukusanya ushahidi wake juu ya mgogoro wa Israel na Palestina na tayari imeanza kuandika ripoti yake.

Kamisheni hiyo ilikuwa inaangalia tabia ya pande zote husika katika mgogoro huo, Israel na Hamas ambalo ni vuguvugu la kiislamu linalodhibiti ukanda wa Gaza linalotaka kusambaratika kwa Israel.

Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kamisheni hiyo ya Umoja wa Mataifa inayochunguza mgogoro wa Israel na Palestina inapaswa kufutiliwa mbali kufuatia mkuu wake kujiuzulu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/G. Tibbon

Benjamin Netanyahu amesema ni wazi kwamba tume hiyo ilioundwa na baraza la kutetea haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa inaipinga Israel na imeonesha kutokuwa na nia yoyote ya kutetea haki za binaadamu.

Israel inasemekana kutotoa ushirikiano kwa tume hiyo ikitoa sababu ya tume hiyo kuionea Israel na kwamba tayari ilionekana kulemea upande mmoja na majibu yake ya mwisho yalikuwa yanajulikana yatachukua muelekeo gani.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP

Mahriri: Mohammed Abdul Rahman