Westerwelle-Balkans
26 Agosti 2010Akiwa katika ziara yake ya kwanza kwenye nchi hiyo ya eneo la Balkans amezungumzia juu ya msimamo wa Ujerumani wa kutokubaliana na azimio la Serbia ililoliwasilisha mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa.Azimio hilo linataka pafanyike mazungumzo zaidi juu ya suala la uhuru wa Kosovo ambao unapingwa hadi sasa na Serbia pamoja na washirika wake.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akiwa nchini Serbia hii leo ameitaka nchi hiyo kukubaliana na ukweli wa mambo kwamba imelipoteza jimbo lake la zamani la Kosovo,akisema uhuru wa jimbo hilo ni wa halali na ulio wazi kabisa.Mjini Belgrade Westerwelle amewatolea mwito viongozi wa Serbia kulifutilia mbali azimio lao dhidi ya uhuru wa Kosovo ambalo wanatarajia kulipitisha katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Septemba.
Waziri Westerwelle ameiambia Serbia kwamba itakuwa jambo la busara zaidi ikiwa nchi hiyo itaachana na azimio lake na kuanzisha mazungumzuo na jimbo hilo akisisitiza kwamba maridhiano ndio njia pekee inayoweza kufanikiwa ikiwa upande mmoja haukubaliani na ukweli wa mambo.
Serbia inapanga kutafuta uungaji mkono wa azimio lake ambalo limewatia katika mvutano na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya.Nchi 22 za Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani zinautambua uhuru wa Kosovo. Azimio la Serbia linalaani hatua ya Kosovo ya kujitangazia uhuru ingawa mahakama ya sheria ya kimataifa ICJ mwezi wa July ilitangaza hatua hiyo ya Kosovo kuwa halali na kutaka paanzishwe upya mazungumzo juu ya suala hilo.
Msimamo wa mahakama ya ICJ ulifikishwa katika Umoja wa mataifa na serikali ya Kosovo inatarajia kwamba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litaunga mkono uhuru wake licha ya upinzani wa Serbia.
Aidha waziri wa mambo ya nje Westerwelle akizungumza katika chuo kikuu cha Belgrade amesema kwamba Serbia kama nchi nyingine za magharibi za eneo la Balkan zina nafasi ya kujiunga katika Umoja wa Ulaya ingawa ameonya kuwa safari ya kuelekea katika chombo hicho ni ngumu na nzito.
Baada ya mazungumzo na waziri mkuu Mirko Cvetkovic Westerwelle alisema kwamba mustakabali wa nchi za balkans utatokana na Umoja wa Ulaya lakini akasisitiza kwamba Umoja huo hauwezi kuwakaribisha wanachama ambao wanachochea mizozo ya nje.Ujerumani iko tayari kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Serbia na Kosovo ili kuutatua mvutano uliopo.Uhuru wa Kosovo umetambuliwa na nchi 69 ikiwemo nchi zenye nguvu duniani isipokuwa Urussi na China.
Waziri huyo wa Ujerumani aliwasili Belgrade leo asubuhi akitokea Zagreb na amepangiwa kuelekea Bosnia baadae hii leo na hatimae kuitembela Kosovo hapo kesho ijumaa kituo chake cha mwisho katika ziara yake hiyo ya nchi za iliyokuwa Yugoslavia.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri Josephat Charo